Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amezindua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuweka mawe ya msingi kwa miradi hiyo, ikiwemo shule za sekondari, masoko ya kisasa, hospitali, na nyumba za watumishi. Hii ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya miradi mkoani Pwani.
Katika siku ya pili ya ziara hiyo, Mhe. Bashungwa alitembelea Halmashauri ya Mji Kibaha, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha DC, na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze. Alifanya uwekaji wa mawe ya msingi katika shule tano za sekondari, ambapo mbili ziko katika Halmashauri ya Kibaha Mji, moja katika Halmashauri ya Kibaha DC, moja katika Halmashauri ya Chalinze, na nyingine katika Halmashauri ya Bagamoyo.
Aidha, Waziri Bashungwa aliweka mawe ya msingi katika masoko mawili, Soko la Kisasa la Mlandizi na Soko la Bwilingu, yaliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze. Pia, alizindua rasmi ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kibaha DC pamoja na nyumba nane za watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
Baada ya uwekaji wa mawe ya msingi kwa miradi hiyo, Mhe. Bashungwa alitatua changamoto kadhaa zilizokuwa zinakwamisha miradi hiyo, ikiwemo barabara na upatikanaji wa maji katika maeneo husika.
Waziri Bashungwa alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kutenga trilioni 1.3 kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wa Pwani. Alimpongeza pia Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, kwa usimamizi thabiti wa utekelezaji wa miradi hiyo, ambayo inaendana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika mikutano ya hadhara aliyoifanya na wananchi, Waziri Bashungwa aliwahamasisha kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, ili waweze kuchagua viongozi sahihi katika uchaguzi ujao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.