Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist W. Ndikilo amesema chama cha msingi cha korosho (AMCOS )ama wataalam wa kupima ubora wa korosho, kitakachobainika kufanya mchongo na udanganyifu katika msimu huu wa ununuzi kitachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufungwa. Aidha amewasihi Wakuu wa Wilaya zote Mkoani Pwani, kusimamia na kuweka mazingira wezeshi ili msimu uwe na mafanikio makubwa. Hata hivyo, amemtaka Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na uzalishaji Mkoani Pwani, Bw. Shangwe Twamala kusimamia mnada wa ununuzi wa korosho unaoanza rasmi Novemba 8 mwaka 2017 Mkoani Pwani kwa uwazi ili kuondoa malalamiko.
Akifunga kikao cha tathmini na maandalizi ya msimu mpya wa zao hilo la kibiashara, Mwenyekiti wa kikao hicho, Mhandisi Ndikilo, alisema hatokubali mnada huo kugeuzwa kuwa ni dili. Aliziasa AMCOS na wataalamu wa kupima ubora kuepukana na na udanganyifu kwenye ubora wa korosho. “Kumekuwepo na udanganyifu mkubwa unaofanyika katika maghala ya kuhifadhia korosho ambapo baadhi za AMCOS zimebainika kusababisha uzito wa korosho zilizopimwa kwenye maghala, Ambapo kabla ya mnada hupungua kwa kiasi kikubwa wakati mnunuzi anapokabidhiwa korosho hizo” alielezea.
Mhe. Ndikilo alieleza kuwa, Wilaya ya Mafia ina tani 200 za korosho na katika mnada wa Novemba 8 kutakuwa na tani 50 kutoka wilaya hiyo. Mkoa wa Lindi na Mtwara mnada umeshaanza hivyo hataki kusikia kisingizio katika mnada huo. Katika hatua nyingine, aliitaka bodi ya korosho kupeleka magunia Mkoani hapo, kwani yaliyopo hayatoshi na kusababisha athari kwa wakulima na kuhofia kukosa faida.
Mhandisi Ndikilo alisema, kutaimarishwa vizuia vya kudhibiti utoroshwaji wa korosho nje ya Wilaya na Mkoa . Alikemea biashara ya korosho kufanywa katika mfumo wa kangomba ambao huwakandamiza wakulima wa zao hilo. Mhandisi Ndikilo, alisema korosho zote zitakazokutwa kwenye magari yatakayokamatwa yakiwa kwenye mifumo isiyo rasmi badala ya stakabadhi ghalani ambao unatambulika, korosho hizo zitataifishwa na mtuhumiwa atakamatwa na Jeshi la Polisi.
Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Mhe. Filberto Sanga alisema zao la korosho ni zao la biashara ambalo linanufaisha mkulima na taifa kwa ujumla. Alisema kutokana na umuhimu huo halipaswi kufanyiwa ujanjaujanja kwa watu kujinufaisha zaidi ya mkulima husika. Mhe. Sanga alieleza kwamba, korosho za baadhi ya wakulima zipo chini kwenye maji zinaharibika kwa kukosa magunia ya kuzihifadhi. Nae mwenyekiti wa CORECU Mkoani Pwani, Bw. Rajabu Ng’onoma alisema awali waliagiza magunia ya ziada ambayo waliyahifadhi kwenye ghala lao la CORECU.“Tulijua yatatosheleza na yanaweza kutumika na kubaki lakini hapo kipindi cha kati ilitokea tatizo juu ya magunia hayo ambapo wanaodaiwa kuhusika wameshakamatwa na kwasasa wanauachia mhimili lengwa uchukue mkondo wake ” alifafanua Ng’onoma . Bw. Ng’onoma alisema wanatekeleza majukumu yao kwa uzalendo na uchungu ili kuhakikisha korosho inaleta mapinduzi makubwa na maendeleo chanya Kimkoa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.