Chama Cha Walimu Tanzania(CWT) kimetoa msaada wa fedha taslimu Shilingi milioni tatu 3,000,000/= kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya walimu iliyoathiriwa na mafuriko kwenye Wilaya za Kibiti na Rufiji Mkoani Pwani.
Akikabidhi msaada huo mwanzoni mwa wiki hii ambao utatumika kununua mifuko ya saruji 200 Mtunza Hazina wa CWT Abubakary Alawi alisema, wameamua kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuweka Mazingira mazuri ya kufundishia kwa walimu.
Alawi alisema, pamoja na kuwa CWT ni chama cha kutetea maslahi ya walimu, lakini kwasasa wameamua kuungana katika kusaidia kurejesha miundombinu ya walimu ambayo imeharibiwa na mafuriko.
" Tumeguswa na hali ya taharuki iliyowapata walimu wenzetu wa Rufiji na Kibiti tumekuja kutoa mchango wetu kwako"alisema Alawi.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo alishukuru kwa msaada huo na kuomba makampuni mengine ambayo yamewekeza katika Mkoa huo kuiga mfano wa CWT.
"CWT ni Taasisi inayojitambua inayoshughulika na matatizo ya wananchi na katika hili niwapongeze kwa kuunga mkono juhudi za Serikali"
"Serikali haiwezi kujenga Miundombinu yote kwa wakati mmoja nichukue fursa hii kuwaomba wadau wengine na wamiliki wa Viwanda Pwani kuiga mfano wa CWT wa kusaidia changamoto zilizopo Kibiti na Rufiji" alisema Ndikilo
Mhandisi Ndikilo alibainisha kuwa chanzo cha mafuriko katika Wilaya hizo ni mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimesababisha mabwawa ya Mtera na Kidatu kufunguliwa na hivyo maji kufurika kwenye mashamba na makazi ya watu.
Mwisho, Aliwahimiza Waalimu wa Mkoa Pwani kuendelea kutoa elimu ya tahadhari ya Kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya Corona kwenye maeneo wanapoishi kipindi hiki ambapo Serikali imefunga Shule. "Msichoke kuwaelimisha Wananchi alisema Ndikilo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.