Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ,Dkt.Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Majukwaa ya Wanawake kiuchumi kuwafikia wanawake wote kuanzia Vijijini na pembezoni mwa miji ili waweze kupata fursa za kiuchumi na kuondokana na hali ya kuwa tegemezi ndani ya jamii.
Akizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji majukwaa ya uwezeshaji wanawake Kiuchumi ,kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Kwamfipa Kibaha Mkoani Pwani, alieleza mwongozo huu ukawe kichocheo cha kuyaendeleza majukwaa hayo kwa ustawi wa jamii.
Gwajima alieleza, mwongozo huu utaleta Mapinduzi ya kimaendeleo kwa mwanamke na kuongeza ufanisi na majukwaa kujulikana kuanzia ngazi ya chini ,yatasaidia kuongeza Uelewa kujitegemea kiuchumi na kushughulikia Changamoto za kibiashara.
Alielezea, ni wakati wa kufanya matamasha, kwenda nyumba kwa nyumba kuwafikia wanawake ambao hawafikiki kirahisi waweze kunufaika kiuchumi.
"Tuwafikie wa vichochoroni, Vijijini tufanye Mapinduzi kuwafikia wasiojua fursa zinazotolewa na Serikali,Tusipoangalia hawa wengine watakosa neema za Rais Samia Suluhu Hassan,Tukiwaacha ndio tunawakuta wanaombaomba kwani ukiwauliza unakuta hawajui kama kuna fursa za kiuchumi"alifafanua Gwajima.
Gwajima ,alitoa Rai kwamba mwongozo huo sio agenda ya Kisiasa haihusiki na itikadi za kisiasa bali unalenga kumfikia kila mmoja aweze kunufaika na matunda ya Serikali kiuchumi.
Akitoa salamu Katibu Mkuu wa wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia,wazee, watoto upande wa Zanzibar Mariam Abdallah alibainisha, ni hatua moja ya kushirikiana katika Muungano wetu kuweka haki,usawa kwa wanawake.
"Tunaahidi kwa Zanzibar kwenda kutekeleza mwongozo huu kwa vitendo ili kuhakikisha Wizara zote zinashirikiana kumkomboa mwanamke"anasema Mariam.
Awali Mkurugenzi Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi (NEEC) Bengi Issa alisema, mwaka 2017 Baraza Hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii walitengeneza mpango na kutengeneza kuanzisha majukwaa ya wanawake Lengo kuwakutanisha wanawake kubadilishana uzoefu,kubuni biashara mbalimbali na kutatua changamoto zao kwa umoja.
Alieleza ,hadi Sasa Kuna majukwaa ya wanawake 151 ndani ya Halmashauri nchini, majukwaa 1,354 kata, na 1,859 mitaa na Vijijini.
Bengi alieleza ,mwongozo huo utakwenda kuleta matokeo chanya kwa majukwaa yanayoanzishwa na wanampongeza Rais Samia Suluhu Hassan Kuwa kinara wa kuinua wanawake na makundi maalum kiuchumi.
Alitaka maeneo ambayo bado hayajaanzisha majukwaa hayo kuanzisha ili kuwapa fursa wanawake wajasiriamali kujiinua kimaendeleo na kuweza kunufaika kiuwezeshaji kirahisi kwenye makundi na umoja wao.
Akitoa salamu za jukwaa la wanawake Mkoani Pwani, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake mkoa wa Pwani,Mariam Ulega alifafanua kwamba, mwongozo wa Kitaifa wa uanzishaji na uendeshaji majukwaa utawasaidia kuonyesha njia pale ambapo kulikuwa na mapungufu .
Alisema, kipindi cha nyuma wapo ambao waliyabeza majukwaa haya ,Lakini kwasasa inashuhudiwa mafanikio makubwa yanayopatikana katika majukwaa hayo.
"Tunampongeza Rais Samia,tunamshuhudia halali kuhakikisha anamkomboa mwanamke wa Kitanzania, Tunamuenzi kwa kuunga mkono jitihada zake hizo kuhakikisha tunaendeleza jukwaa la mkoa na kushikana wanawake kutatua changamoto zetu na kusonga mbele"alisisitiza Mariam Ulega.
Mariam Ulega alitaja changamoto za mkoa Kuwa Ni sanjali na elimu ndogo ya usindikaji ,kushindwa kumfikia kirahisi kumkomboa mwanamke anaeishi Vijijini, Watoto wa kike kukatisha masomo kutokana na mimba za utotoni ambazo nyingi zinasababishwa na tamaa na vishawishi wanavyopewa na madereva bodaboda.
Akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Pwani, Mkuu wa wilaya ya Kibaha Sara Msafiri alisema ,kiasi cha sh.Bilioni 2.5 zimekopeshwa kwa vikundi vya wanawake kwa mwaka 2021-2022 ambapo Bilioni 2.3 wamerejesha .
Alisema , kijumla tangu kuanzishwa kwa majukwaa mkoa umeanzisha majukwaa 1,722 kati yake majukwaa 980 yamesajiliwa na kukopeshwa Bilioni tano
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.