Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Dr Delphine Magere amewataka watumishi kuacha tabia ya kukaa ofisini na badala yake wajenge tabia ya kuwafikia wananchi na kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Dr Magere alitoa wito huo Agosti 24,alipokuwa wilayani Mafia na kuzungumza na wakazi wa kata ya Kirongwe wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo aliyoifanya kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi katika Halmashauri za Mkoa huo.
Katibu Tawala huyo alisema kuwa , huu sio wakati wa kukaa na matatizo ya wananchi na kila mmoja anatakiwa kuwajibika ipasavyo kutekeleza wajibu wake bila kusubiri msukumo kutoka ngazi za juu.
"Zama zimebadilika tuache kukaa ofisini tutoke tukawasikilize wananchi tunaowatumikia wakati mwingine wanaotukwamisha ni watumishi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati" alisema
Alisema endapo kila mmoja atasimamia majukumu yake ipasavyo itapunguza uwepo wa kero za wananchi ambazo hazitafutiwi ufumbuzi kwa wakati na kuwafanya wananchi kufanya shughuli za maendeleo na kujikwamua na hali ya umasikini kwenye maeneo yao.
"Tusikae na matatizo ya wananchi tujenge tabia ya kuwasikiliza tutatue kero zao watumishi tutumike, kuanzia ngazi za chini tukifanya hivyo hata viongozi wa juu hawapati shida wanapotembelea maeneo hayo" alisisitiza.
Akiwa Mafia Mkuu huyo wa Mkoa aliahidi Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na Wilaya kusimamia miradi ya maendeleo ambayo haijakamilika kutekelezwa kwa wakati na kuwasaidia wananchi wa maeneo husika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.