Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahil Geraruma amewaasa viongozi, watendaji na wataalamu wa Halmashauri kusimamia fedha za miradi na kujenga tabia ya kuhifadhi nyaraka za ujenzi wa miradi ya maendeleo ili kujiepusha na mkanganyiko wakati wa ukaguzi.
Akikagua miradi ya maendeleo Leo Mei 1, 2022 katika mradi wa Zahanati ya Nyanda Katundu na barabara ya Mji Utete, wilayani Rufiji Mkoani Pwani, Guraruma aliwaasa watendaji hao kufuatilia miradi ya maendeleo kwa maslahi mapana ya wananchi kwenye Maeneo Yao.
Alihimiza kuwa Watumishi wanapaswa kutekeleza miradi kwa uadilifu na kuzingatia usimamizi wa miradi kwa maslahi mapana ya wananchi.
Pia Guraruma alikemea baadhi ya watumishi na viongozi nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani wanasababisha kudorora kwa miradi.
Akikagua mradi wa vijana kikundi cha Kumekucha Umwe Kaskazini, alielekeza Halmashauri kutenga fedha za vijana na kuhakikisha vikundi vinarejesha mikopo kwa wakati lengwa.
Kuhusu suala la Sensa, Bw. Geraruma amehimiza wananchi kujitokeza katika Zoezi hilo Mwezi Agosti mwaka huu kwa Ajili ya mipango ya maendeleo pasipo kupuuzia.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rufiji,John Kayombo alisema, zahanati hiyo imepewa milioni 50 ambapo imebaki zaidi ya milioni Saba na ujenzi utaendelea.
Awali, akipokea mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Lindi, mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, aliweka bayana kwamba jumla ya nyumba 515,668 zimeingizwa kwenye mfumo wa Zoezi la anwani za makazi sawa na asilimia 105.61.
Alisema kufuatia maandalizi ya sensa na makazi wamejipanga na kuendelea kuhimiza wananchi kujitokeza kwenye Zoezi hilo agost mwaka huu.
"Mkoa wetu ulikuwa miongoni mwa mikoa 13 kwenye zoezi la sensa ya majaribio na Tunashukuru limefanya vizuri "Kunenge alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa,kiasi cha sh.milioni 816 .2 kutoka Serikali Kuu kimepokelewa na Halmashauri zimechangia milioni 320.
Pamoja na hayo, Kunenge alieleza mwenge wa uhuru ukiwa Mkoani hapo utapitia miradi 111 yenye gharama ya Zaidi ya Bilioni 69.2.
"Kati ya miradi hiyo miradi 25 itawekwa mawe ya msingi, 22 itazinduliwa, 6 itafunguliwa na 58 kukaguliwa"alifafanua Kunenge.
Akipokea mwenge wa uhuru Mkuu wa wilaya ya Rufiji Edward Gowelle kutoka kwa Mkuu wa mkoa,alisema mwenge ukiwa Rufiji utapitia miradi sita yenye thamani ya milioni 6.5.
Kati ya miradi iliyotembelewa Rufiji ni pamoja na Zahanati Nyanda Katundu, barabara Mji Utete, mradi wa vijana kikundi cha Kumekucha Umwe Kaskazini, Mradi wa Uraghibishaji falsafa ya mwenge,ghala la mwananchi na madarasa ya Sekondari Mkongo.
Mwenge wa uhuru Mei 2 unatarajiwa kupokelewa huko Mkupuka wilaya ya Kibiti.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.