Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahii Geraruma amesisitiza wajawazito kuanza kliniki mapema na kula lishe bora kwa afya ya mama na mtoto na kuwasihi wanyonyeshe watoto ili wawe na virutubisho kutoka kwa mama.
Geraruma alitoa msisitizo huo wakati akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Msorwa kilichojengwa kwa fedha za tozo ya miamala kwa gharama ya shilingi milioni 250.
Kuhusu ujenzi, Geraruma alizitaka Halmashauri kuzingatia maelekezo ya ujenzi wa miradi ambayo hutolewa na Serikali kulingana na mradi husika na kuhifadhi nyaraka za matumizi ya fedha kwa ajili ya ukaguzi.
Amesema kutokuwa na taarifa za fedha kunatia Shaka na kuonyesha Kuwa kuna Mazingira ya upigaji.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Hadija Nasir ameshukuru wananchi na wadau kwa kushirikiana na Serikali kuinua maendeleo ya wilaya hiyo.
Amesema katika miradi iliyopitiwa na Mwenge, ipo ya fedha za Serikali, kodi ya wananchi ikiwa ni pamoja na Fedha za Tozo na UVIKO 19 zilizofanikisha ujenzi wa miradi mbalimbali ambayo ina tija kwa jamii.
Mwenge wa Uhuru umepokelewa katika wilaya ya Mkuranga ukitokea Kibiti ambapo ukiwa wilayani humo umekagua miradi 14 yenye thamani ya Sh. Bilioni 12.8.
Miradi iliyopitiwa na Mwenge Wilayani Mkuranga ni pamoja na wa ujenzi wa kituo kidogo cha polisi Kijiji cha Mwarusembe, kukagua jitihada za mradi wa mapambano dhidi ya malaria na VVU/UKIMWI, kituo cha afya Kilimahewa na kuweka jiwe la msingi mradi wa maji Mkuranga na tank kubwa la maji Mkwalia wenye thamani ya Bilioni 5.500.
Miradi mingine iliyopitiwa ni kukagua kazi za vijana useremala Mkuranga Mjini, barabara ya lami mita 400 Vikindu-Sangatini, mradi wa madarasa ya Uviko19 Mwandege Sekondari na kuweka jiwe la msingi shule shikizi Mpera.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.