Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo, amemtaka Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya Kibiti kuhakikisha ujenzi huo unakwenda na unakamilika haraka.
Aliyasema hayo Wilayani Kibiti wakati wa ziara yake Wilayani humo, ambopo alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa ,Mkandarasi suma JKT anapaswa kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili utoaji wahuduma uweze kuimarika, kwani kwa sasa huduma zinatolewa katika mazingira magumu na gharama kubwaa kutoka na Ofisi kupanga kwenye majengo ya watu binafsi.
“Hakikisheni Jengo hili linakamilika kwa wakati kwani litafanya Halmashauri kutoa huduma bora kwa wananchi pia huduma zitatolewa sehemu moja , tofauti na sasa” alisema Mhandisi Ndikilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Gulamuhussein Kifu alisema kuwa ujenzi unaendelea na thamani ya ujenzi hadi kukamilika itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.3.
Kifu alisema kuwa,Ujenzi huo ambao unafanywa na Suma JKT unaendelea vizuri kwa sasa tayari ujenzi wa majengo ya chini umekamilika na wanatarajia kuweka zege kwa ajili ya kuanza Ghorofa ya kwanza.
“Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk John Magufuli, kwa kupata fedha kwa ajili ya ujenzi huu na utakapokamilika utaondoa adha ya Halmashauri kupanga kwenye majengo ya mtu binafsi “ alisema Kifu.
Alisema kuwa, Ofisi yake na baadhi ya Ofisi ziko kwenye jengo la Idara ya Maji , Ofisi ya Mkurugenzi na baadhi ya Idara wamebanana kwenye jengo la mtu binafsi huku Ofisi nyingine zikiwa sehemu mbalimbali.
“Tutahakikisha ujenzi huu unakamilika kwa wakati ili tuanze kutumia majengo yetu badala ya kupanga mitaani ambako si salama sana , tofauti na kuwa na Ofisi yetu ambayo itarahisisha utendaji kazi tofauti na ilivyo sasa”alisema kifu.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya hiyo Alvera Ndabagoye alisema kuwa hadi sasa wameshampatia mkandarasi kiasi cha shilingi milioni 961.
Ndabagoye alisema kuwa fedha zilizopo benki ni shilingi Bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi huo wa Makao makuu ya Halmashauri, hivyo hakuna tatizo la fedha.
Naye kwa upande wake Msimamizi wa ujenzi huo kutoka Suma JKT Eric Mtayoba alisema kuwa ujenzi ulichelewa kutokana na ukosefu wa umeme, maji ,na barabara ambapo kwa sasa changamoto hizo hazipo tena na wanatarajia kukamilisha ujenzi huo mwanzoni mwa mwaka ujao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.