Halmashauri katika Mkoa wa Pwani zimetakiwa kuhakikisha kuwa fedha zinazotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za lishe zinatumika kama zilivyopangwa. Aidha, zimetakiwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua vibao vya ufuatiliaji wa makuzi ya watoto katika kila kituo cha afya, ili kuhakikisha kuwa watoto wanapata huduma stahiki za lishe.
Ofisa Lishe wa Mkoa wa Pwani, Mecy Mtaita, akizungumza wakati wa kutoa taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024, alibainisha mikakati mbalimbali iliyowekwa ili kufikia malengo ya mkataba huo. Mtaita alieleza kuwa baadhi ya halmashauri zimekuwa zikishindwa kutumia fedha kama ilivyopangwa, hali inayosababisha kudorora kwa utekelezaji wa mipango ya lishe.
"Baadhi ya halmashauri zimefanikiwa kutumia fedha kwa ufanisi, kama vile Halmashauri ya Kibaha Mjini na Kisarawe ambazo zilitumia asilimia 100 ya bajeti zao za lishe. Halmashauri ya Kisarawe ilitumia asilimia 99.5, ambayo pia ni kiwango cha kuridhisha," alisema Mtaita.
Aliongeza kuwa kuna upungufu mkubwa wa vibao vya ufuatiliaji wa makuzi ya watoto, ambapo kibao kimoja kinauzwa kwa kati ya shilingi 250,000 hadi 350,000. Vibao hivi ni muhimu kwani bila ya takwimu sahihi, ni vigumu kufanya maamuzi sahihi katika kupambana na udumavu na ukondefu kwa watoto walio chini ya miaka mitano.
"Ili kufanya tathmini sahihi, ni lazima vituo vya afya viwe na vibao vya kupimia makuzi ya watoto. Kwa sasa tuna asilimia 27 tu ya vibao hivyo, wakati lengo ni kuhakikisha kila kituo kinaweza kufanya tathmini na kuchukua hatua mapema inapohitajika," alisisitiza Mtaita.
Mtaita alieleza kuwa, kuna haja ya kuboresha mipango na bajeti za lishe ili ziweze kuendana na mahitaji halisi ya jamii. Alisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa huduma za lishe zenye ubora na usawa kwa wote.
Pia, alizitaja changamoto za mkoa, ikiwa ni pamoja na idadi ndogo ya shule zinazotumia unga ulioongezewa virutubishi, pamoja na ukosefu wa vifaa vya kupima iodine (iodine test kits) kwa muda mrefu, jambo ambalo limeathiri uwezo wa kupima uwepo wa madini joto katika chumvi zinazotumiwa na wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisisitiza umuhimu wa halmashauri kutoa fedha kwa wakati ili kuhakikisha utekelezaji wa masuala ya lishe unafanikiwa. Alitoa wito kwa viongozi na watendaji wa mkoa kushirikiana kwa karibu ili kuinua maendeleo na uchumi wa mkoa kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.