Tatizo la ukosefu wa mashine ya mionzi katika hospitali ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani limepatiwa ufumbuzi wa kudumu baada ya serikali kununua mashine mpya yenye thamani ya milioni miamoja na hamsini kwa ajili ya matumizi ya hospitali hiyo.
Mganga Mkuu wa wilaya ya Mafia daktari Zuberi Mzige amesema ununuzi wa mashine hiyo umesaidia kuondoa tatizo walilokuwa wanalipata wakazi wa wilaya ya Mafia kutumia gharama kubwa ya usafiri wa ndege kusafirisha wagonjwa kwenda jijini Dar es salaam kwa ajili kupatiwa vipimo vya mionzi.
Hayo yamebainika wakati wa Ziara ya kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani walipotembelea Wilayani ya Mafia kwa lengo la kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama hicho katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya serikali ya awamu ya tano.
Katika ziara hiyo kamati hiyo ilitembelea hospitali ya wilaya ya Mafia na kukagua mashine mpya ya mionzi iliyonunuliwa na Serikali kwa lengo la kuwaondolea adha wakazi wa wilaya hiyo kutumia gharama kubwa kusafirisha wagonjwa kwa njia ya ndege kwenda jijini Dar es salaam kwa ajili ya vipimo vya mionzi.
Akizungumza na kamati hiyo mganga Mkuu wa wilaya ya Mafia daktari Zuberi Mzige amesema ununuzi wa mashine hiyo imekuwa ukombozi kwa wakazi wa visiwa vya Mafia .
Daktari Zuberi alisema kuwa fedha za ununuzi wa mashine hiyo yenye thamani ya milioni miamoja na hamsini imetolewa na serikali pamoja na ofisi ya mbunge ambapo kati ya fedha hizo milioni hamsini zimetolewa na halmashauri ya wilaya ya Mafia na shilingi milioni miamoja zimetolewa na mbunge wa jimbo la Mafia Mhe. Ramadhani Dau. Doktari Zuberi amesema hayo wakati ziara ya kikazi ya Siku tatu ya kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani ilipotembelea hospitali utekelezaji wa ilani ya CCM katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya serikali ya awamu ya tano.
Akizungumza baada ya kukagua hospitali hiyo mwenyekiti Wa CCM mkoa wa Pwani Mhe. Ramadhani Maneno amesema wameridhishwa na jinsi mkoa huo ulivyotekeleza kwa mafanikio makubwa ilani ya CCM kwa kuboresha upatikanaji Wa huduma za afya pamoja na kuimarisha miundombinu ya vituo vya afya, ,barabara,,maji na ujenzi wa viwanda.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evaristi Ndikilo amesema katika kipindi cha miaka miaka miwili na nusu cha serikali ya awamu ya tano, mkoa wa Pwani umefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ambapo katika kipindi hicho zaidi ya vituo saba vya afya vimepatiwa shilingi milioni 450 kwa kila kituo kwa ajili ya upanuzi na ukarabati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.