Wananchi wa Mkoa wa Pwani watanufaika na ajira na huduma mbalimbali za kijamii baada ya kuzinduliwa kwa hoteli mpya ya The Mayborn iliyopo Mtaa wa Lulanzi, Kata ya Picha ya Ndege katika Manispaa ya Kibaha.
Hoteli hiyo, iliyofunguliwa rasmi Septemba 4, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, inatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo na mkoa mzima.
Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli hiyo, Fikirini Mushi, alisema ujenzi wa hoteli hiyo ulianza mwaka 2010 baada ya kununua ardhi mwaka 2009, ukidhaminiwa na Benki ya Biashara ya NBC. Alieleza kuwa lengo kuu la uwekezaji huo ni kuleta huduma za kiwango cha juu karibu na wananchi, badala ya wao kulazimika kusafiri Dar es Salaam.
“Huduma zitakazopatikana hapa ni pamoja na malazi ya kisasa, kumbi za mikutano na harusi, pamoja na maeneo ya biashara ambayo yatapunguza gharama na muda wa wananchi kufuata huduma hizo mbali,” alisema Mushi.
Akaongeza kuwa hoteli hiyo itafungua fursa za ajira kwa wakazi wa Kibaha na maeneo jirani, kukuza mapato ya Halmashauri kupitia kodi, na kuhamasisha wawekezaji wengine kuwekeza Pwani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema Serikali inaunga mkono uwekezaji huo na kueleza kuwa ni sehemu ya mpango wa kukuza uchumi wa mkoa huo kwa kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja.
“Uwepo wa hoteli hii unasaidia kuondoa changamoto ya wawekezaji kulazimika kuishi Dar es Salaam. Sasa wanapata huduma kwa ukaribu na kwa hadhi ya Manispaa ya Kibaha,” alisema Kunenge.
Hata hivyo, Mushi alitaja changamoto ya miundombinu ya barabara, hasa nyakati za mvua, lakini akaeleza kuwa ana imani Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji.
Hoteli ya The Mayborn inatazamwa kuwa kichocheo cha maendeleo ya sekta ya huduma, ajira na biashara katika Mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.