Idadi ya watu wazima wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu nchini imepungua kutokana na Serikali kuanzisha program mbalimbali kuliwezesha kundi hilo kupata maarifa.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Kongamano la kitaifa la Maadhimisho ya Juma la Elimu kwa watu wazima, Dkt. Sempeo Siafu linalofanyika kitaifa mkoani Pwani.
Amesema, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni - UNESCO, idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu imepungua tangu nchi ya Tanzania ipate uhuru, kutokana na hali hiyo Wizara ya Elimu ilianzisha program maalum kwa ajili ya kuwasaidia watu wazima na vijana waliositisha masomo kurudi shule.
“Hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alianzisha kampeni mbalimbali zinazohamasisha wananchi kujua kusoma na kuandika, na ukiangalia tulikotoka na sasa tumerudi nyuma, natoa rai kuweka mikakati ya pamoja ili kuondoa changamoto hii nchini, taifa la watu walioelimika ni rahisi kuleta maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Siafu.
Ameeleza kuwa, program ya Elimu ya awali itaendelea kufanya vizuri endapo watu wazima watajua kusoma na kuandika kwa ajili ya ushirikiano baina yao na walimu katika kufuatilia maendeleo ya watoto shuleni.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Msingi, Josephat Luoga amesema, Serikali imekuwa ikitekeleza program mbalimbali za elimu ya watu wazima ili kuongeza idadi ya watu wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Amezitaja program hizo kuwa ni Mpango wa Elimu Msingi kwa walioikosa MEMKWA, Mpango wa Elimu Sekondari kwa njia mbadala, Mpango wa Elimu changamani walio nje ya shule, uzalishaji mali, shughuli za ugani na vikundi vya kuweka na kukopa - VICOBA.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Watu Wazima, Elimu Maalum na Michezo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, Ernest Hinju amesema wanao mtandao wa kutosha kuhakikisha kila mtu mzima mwenye lengo la kusoma atapata elimu hiyo katika eneo lake.
Afisa Elimu mkoa wa Pwani, Sarah Mlaki amesema mkoa huo unatekeleza programu mbalimbali kwa halmashauri zote kama vile Mpango wa Elimu ya Msingi kwa waliokosa - MEMKWA, jumla ya wanafunzi 1943 wakiwemo wavulana 1117 na wasichana 826 wamenufaika nao.
Ameongeza kuwa mkoa huo, unatekeleza program ya Mpango wa Uwiano kati ya Elimu ya watu wazima na Jamii - MUKAJE yenye jumla ya wanafunzi 2080 ikitajwa kuwa program nzuri ya elimu nje ya mfumo rasmi kwani wanajifunza na shughuli za uzalishaji mali kama vile mapishi, ushonaji, mapambo, ufumaji, ususi na usindikaji.
Baadhi ya wanufaika wa programu ya Elimu ya watu wazima akiwemo Siri Kibinde amesema kwa sasa amejua kusoma na kufanya shughuli za ujasiriamali kama vile ushonaji, mapambo, ususi na usindikaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.