Wananchi mkoani Pwani wametakiwa kufichua watu wanaojihusisha katika matumizi ya madawa ya kulevya ikiwa ni pamoja na wasambazaji na wauzaji ili kupunguza tatizo la kuweka rehani baadhi ya vijana ambao ndio nguvu kazi .
Akizungumza Chalinze,Bagamoyo mkoani Pwani ,wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru ,kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa ,Charles Kabeho alisema ,matumizi ya madawa hayo ni janga kubwa ndani ya jamii.
“Nawaomba wananchi msiogope kuwafichua wahusika hata kama ni ndugu yako ,jirani, kwani wanaojiingiza katika wimbi hilo wapo miongoni mwetu”
“Jengeni ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo jeshi la polisi ,ili hali kukabiliana na tatizo hili” alisisitiza Kabeho.
Aidha aliwaasa Vijana walioathirika na madawa hayo kuwa wajitambue kwa kuacha ,wasikate tamaa,kwani wanaweza kufanya biashara ndogondogo kwa lengo la kujipatia kipato.
Awali mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ,Alhaj Majid Mwanga akipokea mwenge wa uhuru kutokea Kibaha Mjini alisema, mwenge huo utapitia miradi 15 iliyogharimu sh.bilioni 121.459.3.
Pamoja na hayo ,Alhaj Mwanga alieleza Chalinze pia ni halmashauri inayoongoza kwa makusanyo ya mapato ya ndani kwa zaidi ya asilimia 100.
Mkoa wa Pwani ulipokea mwenge wa Uhuru 12 July mwaka huu kutokea Dar es salaam ,ambapo ulipitia miradi ya maendeleo 67 yenye thamani ya sh.bilioni 162.440.8, kupitia wilaya saba na halmashauri tisa.
Kati ya miradi hiyo miradi 16 iliwekwa mawe ya msingi ,miradi 12 kati ya 13 iliyolengwa kuzinduliwa ilizinduliwa ,nane ilifunguliwa na miradi 21 imekaguliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.