Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu ,Charles Kabeho amemuagiza mtendaji mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na watendaji wake kwenda kufanya ukaguzi katika kiwanda cha Kuchi Jogoo kilichopo kata ya Visiga ,Kibaha mkoani Pwani ili kujiridhisha na kutoa kibali cha kuanza kuzalisha unga wa nafaka .
Pia amewataka wahakikishe wanatimiza agizo hilo mwisho July 26 mwaka huu na apatiwe majibu .
Kabeho aliyasema hayo ,wakati mwenge wa Uhuru ulipokuwa ukikabidhiwa Mkoani Morogoro ukitokea Mkoani Pwani .
Alieleza endapo watachelewa kufanya hivyo watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha alieleza kuwa, wakati alipokwenda kuweka jiwe la msingi kiwandani hapo (july 19) alitoa siku saba kwa shirika hilo liwe tayari litimize agizo hilo .
Kabeho alisema kuwa “,haiwezekani kiwanda kikawa tayari kimekamilisha taratibu za uzalishaji huku TBS ikawa kikwazo cha kushindwa kwenda kukagua na kutoa kibali cha uzalishaji.
“Mradi huo mkubwa wenye gharama ya sh. milioni 812.7 ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhimiza uwekezaji ,inapotokea watendaji wa chombo cha Serikali chenye dhamana ya kuhakikisha lengo la uwekezaji linafanikiwa wanakuwa kikwazo ni jambo linaloumiza na kusikitisha sana” alisema Kabeho.
Kiongozi huyo wa mbio za mwenge kitaifa alisema kwamba ,kila mmoja atimize wajibu wake ili kuunga mkono juhudi za serikali pasipo kuweka vizuizi ambavyo vinaashiria rushwa.
Katika hotuba yake Kabeho alisema kuwa viwanda vinasaidia kutoa ajira kwa Wananchi wetu na kuinua uchumi na pato la Taifa kwa ujumla .
Aidha aliupongeza mkoa wa Pwani kwa kuweza kutekeleza kwa vitendo sera ya kuifanya Tanzania kuwa Nchi ya viwanda.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.