Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu, Charles Kabeho amewataka wananchi kuchapa kazi na wengine kuanzisha uwekezaji mdogo ili kupambana na tatizo la ajira na kupiga vita umasikini.
Pia amewaasa wazazi na walezi ambao watoto wao hawana nafasi ya kuendelea na kiwango cha elimu ya sekondari ,kuwapeleka katika shule za ufundi na veta ili kupata ujuzi mbalimbali,utakaowasaidia kujiajiri.
Hayo ameyasema baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea mradi wa shamba la ng’ombe wa maziwa (Soga daily farm) lililopo Bokomnemela ,Kibaha Viijijini ambapo mradi huo umegharimu kiasi cha sh.bilioni tano.
Kabeho alisema wakati tukielekea kwenye uchumi wa kati ,kuna kila sababu ya kujiongeza kuanzisha biashara ,viwanda vidogo vidogo vitakavyoinua uchumi na kunufaisha wasio na ajira .
Pia alieleza ni vyema jamii ikaweka msukumo kwa vizazi vyao kujiendeleza katika ufundi ili kuzalisha wataalamu watakaoweza kuviendeleza viwanda vinavyojengwa.
Pamoja na hayo ,kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru alikemea matumizi ya madawa ya kulevya na usambazaji kwani huathiri nguvu kazi ya Taifa hasa vijana .
Aliwasihi vijana kujiepusha na kukaa vijiweni na badala yake wajituma kwa kufanya kazi na biashara ndogondogo ,ili kuendana na kasi ya awamu ya tano.
Hata hivyo Kabeho ,alitaka baadhi ya watu kuacha kuzungushia bustani zao vyandarau vyenye dawa na badala yake wavitumie kwa ajili ya matumizi lengwa.
Alisema kuwa ,ugonjwa wa malaria bado upo ambapo waathirika zaidi ni wajawazito na watoto chini ya miaka mitano .
Awali akitoa taarifa ya shamba la ng’ombe wa maziwa, daktari wa Soga daily farm, Omary Batenganya alisema, lilianza mwaka 2014 likiwa na ng’ombe 395 ,sasa lina ng’ombe 1,010 na kondoo 235.
Alielezea lengo la kuanzisha shamba hilo ni kuzalisha maziwa mengi na kutoa ajira.
Batenganya alisema ,ng’ombe mmoja kwa siku anakamuliwa lita 15 -30 kwa kwa mkupuo .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.