Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Nsajigwa George, leo Julai 18, 2025, ameongoza ufunguzi rasmi wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Mpango Kazi wa Pili wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II) kwa mwaka 2024/2025 hadi 2028/2029. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kibaha.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Nsajigwa ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana kikamilifu na Serikali katika utekelezaji wa mpango huo kwa kuhakikisha kuwa Kamati za MTAKUWWA zinaanzishwa na kuimarishwa kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa hadi taifa.
Nsajigwa alibainisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Kwanza (MTAKUWWA I) umeleta mafanikio makubwa, ikiwemo kupungua kwa matukio ya ukatili wa kimwili kwa wanawake kutoka asilimia 40 mwaka 2015 hadi asilimia 27 mwaka 2022, ukatili wa kingono kutoka asilimia 17 hadi 12, na visa vya ukeketaji kutoka asilimia 10 hadi 8.
“Mafanikio haya yametokana na juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau mbalimbali, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, pamoja na OR-TAMISEMI,” alisema Nsajigwa.
Aidha, alieleza kuwa Serikali imeongeza huduma za mikopo yenye masharti nafuu kupitia mifuko mbalimbali, ikiwemo asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Lengo ni kuwawezesha kiuchumi ili kupunguza ukatili unaochochewa na hali ngumu ya maisha.
Katika kipindi cha MTAKUWWA I, jumla ya Kamati 18,186 za Ulinzi wa Wanawake na Watoto ziliundwa nchi nzima, huku Mkoa wa Pwani ukiunda Kamati 756 sawa na asilimia 93.5 ya lengo.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio, alisisitiza umuhimu wa ulinzi wa mama na mtoto akisema, “Kumlinda mama ni kupunguza asilimia 75 ya matatizo ya mtoto.” Aliongeza kuwa maboresho ya miundombinu ya afya yamechangia utoaji wa huduma bora kwa waathirika wa ukatili na kusaidia kubadilisha mitazamo hasi katika jamii.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Pwani, Bi. Grace Tete, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mikopo ya asilimia 10, alisisitiza umuhimu wa wanufaika kubuni biashara zenye tija zinazokidhi mahitaji ya soko ili kujitegemea kiuchumi na kufungua fursa zaidi za kifedha.
Mpango huu wa Pili wa Taifa (MTAKUWWA II) ni mwendelezo wa jitihada za kitaifa kuhakikisha wanawake na watoto wanalindwa, wanathaminiwa na kuwekewa mazingira salama ya kuishi na kuendeleza maisha yao kwa ushirikiano wa jamii nzima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.