Serikali imetatua kero ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya Sekondari kutoka Kijiji cha Kilimahewa kwenda Kiimbwanindi wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.
Hayo yamebainika Mkuranga leo Novemba 8, 2023, katika muendelezo wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge anayetembelea na kukagua miradi ya maendeleo Mkoani humo.
Kutokana na kero hiyo iliyodumu kwa muda mrefu, Serikali ilianza ujenzi wa shule ya Sekondari ya kutwa Kilimahewa ili kuondoa kadhia hiyo.
Taarifa ya utekelezaji mradi huo inaeleza kuwa ujenzi huo kwa sasa umefikia asilimia 92 na kuwa unatarajiwa kukamilika wakati wowote mwezi huu na kugharimu kiasi cha sh. milioni 528.9.
"Mmemtendea haki Mhe. Rais, mmetuheshimisha kukamilisha ujenzi huu, ni shule bora miongoni mwa shule zilizo bora," alieleza Kunenge.
Awali mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutawezesha zoezi la ufundishaji na kujifunza kukamilika kiufasaha kutokana na miundombinu hiyo.
"Tunaishukuru Serikali kutuletea fedha nyingi hapa Mkuranga, awali watoto walikuwa wakitembea masafa marefu ili kufika Mkamba Sekondari, uwepo wa shule hii sasa unaondoa adha hiyo na tunashukuru inaenda kukamilika kwani tumefikia asilimia 80 ya utekelezaji," amesema DC Hadija na akaahidi kufanya usimamizi ili ujenzi huo ukamilike ndani ya wiki mbili.
Awali, akitoa taarifa ya mradi wa shule hiyo, Kaimu Mkuu wa shule ya Sekondari ya kutwa Kilimahewa, Rabii Athumani alifafanua kuwa, shule ilianza machi 2023 baada ya kupata usajili.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amekagua ujenzi wa shule ya Sekondari Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo Shungubweni, ambao utagharimu shilingi milioni 595.
Akiwa Mkuranga Mkuu huyo wa Mkoa ametembelea pia kiwanda cha kubangua korosho kata ya Kiparanganda (Sabayi Agroprocessing Ltd. na akakagua ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa km.0.5 pamoja na kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.