Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt.Jakaya Kikwete amewaasa wenye viwanda Mkoani Pwani na nchi kijumla kuzalisha bidhaa bora zinazolingana na soko la ushindani katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kujiinua kimasoko.
Aidha ameutaka mkoa huo kuboresha Mazingira ya Uwekezaji na kusimamia maeneo yanayotengwa kwa ajili ya uwekezaji (kongani) kwa kuzingatia maendeleo yanavyokuwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
Akifungua maonyesho ya tatu ya wiki ya biashara na uwekezaji Mkoani Pwani yanayofanyika Mailmoja Kibaha Mjini,Kikwete alieleza Tanzania ni miongoni mwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki ambapo zipo nchi saba hivyo Kuna kila sababu ya kuzalisha bidhaa zenye viwango na ubora .
"Hatua tuliyofikia tupo katika ushindani Lazima tuzalishe bidhaa zetu na kuwa bora ,nchi yetu imesaini Africa Continental free trade area ,biashara huru Afrika ,mtakuja kusema Serikali izue bidhaa zinazojiuza Lakini tutashindwa kwakuwa mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itafungua "
"Tuhakikishe tunazalisha bidhaa Bora vinginevyo itakula kwetu,hata kama tunazalisha kibongobonho lakini hao wabongo wanataka bidhaa bora pia"alisisitiza Kikwete.
Hata hivyo Kikwete alisema ,Uchumi unakuwa kwa uwekezaji Kama hakuna uwekezaji hakuna uchumi na utakwama na kusinyaa.
Vilevile aliwashauri kusimamia Maeneo wanayojenga viwanda ,kwani vipo viwanda vilivyojengwa wilayani Mkuranga ambavyo vipo barabarani kulingana na mahitaji na maendeleo yanavyokuwa vinaweza kuja kumegwa kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara.
Kikwete alimpongeza mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge kwa kutenga maeneo ya uwekezaji,kongani za viwanda.
Katika hatua nyingine Kikwete alisema Serikali inafanya kazi nzuri,katika kuinua sekta ya uwekezaji na viwanda na kuimarisha Mazingira bora ya uwekezaji.
"Tumeona Mamlaka ya maji safi na maji taka (DAWASA) wanavyoweka nguvu kubwa ya kuboresha miundombinu ya maji safi na salama na kufikisha kwenye maeneo ya uwekezaji , Serikali imejenga reli ya kisasa (SGR), imeongeza huduma za usafiri wa anga na vingine vimejengwa na kujenga kongani za viwanda."
Alisema uwekezaji una manufaa makubwa katika kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja ,ambapo itasaidia vijana kupata ajira na kuondokana na kushinda kucheza pool.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Pwani Mhe Abubakari Kunenge alieleza mkoa una viwanda 1,460 kati ya hivyo 90 ni vikubwa.
Alieleza kwamba ,mkoa huo imejipanga katika sera ya uwekezaji na viwanda kwa kutekeleza kwa vitendo .
"Ukitaka kuwekeza njoo Mkoani Pwani,tumejipanga kwa kuweka Mazingira Bora na ulinzi na Usalama ,tumeboresha miundombinu ya barabara,maji,umeme kwa ajili ya viwanda"
"Pia kwa kuzingatia masuala ya uwekezaji na changamoto zao mkoa tumetenga kila siku ya Jumanne tuna Taasisi 19 ambazo zinasikiliza kero za wawekezaji na kuzitafutia ufumbuzi"alisema Kunenge.
RC Kunenge alielezea Kuwa ,katika uwekezaji wamesheheni kwenye nyanja zote ikiwemo kilimo, biashara, ufugaji,uchumi wa blue (utalii) Kuna fukwe yenye km.1,132 kwa ajili ya uwekezaji,Kuna saadan, selou iliyopo Rufiji ambapo mkoa una jumlanya vivutio 72.
Akifafanua zaidi Kunenge alisema ,upande wa maji kwa wawekezaji na kusambaza maji kwa jamii RUWASA na DAWASA mkoa zinafikisha maji kwa asilimia 86.
Anasema Serikali ilipeleka Bilioni 197 kwa Ruwasa na DAWASA kwa ajili ya kuhakikisha inasogeza huduma ya maji ndani ya mkoa na hatua mbalimbali za zinaendelea huku miradi mingine ikiwa imekamilishwa.
Alitoa rai kwa Watanzania kupenda na kuvienzi viwanda vidogo vidogo lakini pia kununua bidhaa zinazozalishwa katika viwanda hivyo ili kuviwezesha viweze kupiga hatua zaidi.
Maonyesho ya tatu ya wiki ya biashara na uwekezaji Mkoani Pwani,yalianza mwaka 2018 akiwa mkuu wa mkoa wakati huo Evarist Ndikilo ,na haya ya Sasa ni Mara ya tatu ambapo yameandaliwa na mkoa kwa kushirikiana na SIDO ,kuratibiwa na Tantrade na wafadhili wakuu ni SINOTAN.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.