“Mkandarasi atakaesaini mkataba hapa mtuachie sisi serikali ya Mkoa kumfatilia, tunakuahidi tutamfatilia usiku na mchana na yeye afanye kazi zake usiku na mchana kulingana na mkataba unavyosema ili kuhakikisha wananchi wa Kisarawe wanapata maji safi na Salama”
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Everist Ndikilo mwanzoni mwa wiki hii wakati akitoa salam zake katika hafla ya uwekaji wa saini mkataba wa ulazaji bomba la maji kutoka Kibamba kwenda Kisarawe .
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa ,upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Kisarawe utasaidia kufungua fursa nyingi za uwekezaji hasa uwekezaji wa Viwanda na kuchochea uchumi na mji huo.
“Mh. Waziri mimi nauona mji wa Kisarawe ulikuwa umedumaa, lakini upatikanaji wa maji katika mji huu utapelekea mji huu kukua na kutanuka vizuri”alisema Ndikilo.
Aidha Mhandisi Ndikilo alisema kuwa katika Wilaya ya Kisarawe ipo miradi 141 ya maji ya visima virefu na vifupi ambavyo vipo mbioni kukamilika, hivyo kukamilika kwa visima hivi na mradi huo wa ulazaji wa bomba la maji utasidia upatikanaji wa maji kwa kiasi kikubwa katika Wilaya ya Kisarawe.
Katika Hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Mh Dkt John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa maelekezo aliyoyatoa siku ya tarehe 22 Juni 2017 wakati wa uzinduzi wa mradi wa maboresho wa bomba la maji la kutoka Ruvu kwenda Dar es salaam baada ya kumpa taarifa ya ukosefu wa maji kwa kipindi kirefu katika wilaya ya Kisarawe.
Naye waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe, alisema kuwa mradi wa ulazaji bomba la maji Kisarawe utasaidi kupatikana kwa maji ya kutosha na utapelekea kukua kwa mji wa kisarwe kubadilika na kuwataka wananchi waweze kuulinda na kuuenzi mradi huo.
Mradi huo wa ulazaji wa bomba la maji kutoka kibamba kwenda Kisarawe umetiwa saini baina ya kampuni ya China Henan International cooperation group na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania unatarajiwa kutekekezwa kwa muda wa miezi 15.Utiaji sahihi huo ulishuhudiwa na waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Mhandisi Isack Kamwele na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Mh. Suleiman Jafo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.