Mkoa wa Pwani umeongeza kivutio kipya cha utalii na uwekezaji baada ya kuzinduliwa rasmi kwa hoteli ya kisasa ya The Mayborn iliyopo Mtaa wa Lulanzi, Kata ya Picha ya Ndege katika Manispaa ya Kibaha.
Hoteli hiyo, iliyofunguliwa Septemba 4, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, inatarajiwa kuongeza hadhi ya Kibaha kama kitovu cha kibiashara na mapokezi ya wageni wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Kunenge alisema uwepo wa hoteli hiyo unasaidia kupunguza utegemezi wa Dar es Salaam pekee kama sehemu ya kupokea wageni wa kibiashara na wawekezaji, kwa kuwa sasa huduma za kiwango cha juu zinapatikana Pwani.
“Wawekezaji na wageni wengi waliokuwa wanalazimika kulala Dar es Salaam sasa wanaweza kupata huduma zote muhimu Kibaha, jambo litakaloongeza mapato na kukuza utalii wa ukanda huu,” alisema Kunenge.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli hiyo, Fikirini Mushi, alisema ujenzi wake ulidhaminiwa na Benki ya Biashara ya NBC baada ya kununua ardhi mwaka 2009 na kuanza ujenzi mwaka 2010.
Alisema licha ya changamoto za miundombinu ya barabara, hoteli hiyo imekamilika na imejipanga kutoa huduma za kisasa ikiwemo malazi ya kifahari, kumbi za mikutano na harusi, pamoja na maeneo ya biashara.
“Lengo letu ni kuifanya The Mayborn kuwa chaguo la kwanza kwa wageni wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea Pwani, na kuifanya Manispaa ya Kibaha kuwa na hadhi ya kimataifa,” alisema Mushi.
Hoteli hiyo inatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa sekta ya huduma na kuongeza mvuto wa Mkoa wa Pwani kama kitovu cha uwekezaji, biashara na utalii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.