Serikali Mkoani Pwani kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa zao la Mhogo wameazimia kwa pamoja kujenga ujenzi wa kiwanda kikubwa kwa ajili ya kuchakata zao la Muhugo ambacho kitajengwa katika eneo la Chailinze lililopo halmashaurli ya Chalinze Wilayani Bagamoyo kwa lengo la kuwakomboa wakulima wa zao hilo ili kuondokana na chanagamoto zinazowakabili katika upatikaniji soko.
Maazimio hayo ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zao hilo la Muhogo yamefanyika katika mkutano wa wadau wa zao la muhogo katika Mkoa wa Pwani ambacho kimeweza kuwajumuisha viongozi mbali mbali wa serikali pamoja na wadau wa zao hilo wakiwemo wakulima kwa lengo la kuweka mikakati na kujadili changamoto zinazowakabili wakulima hao wa zao la muhugo.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kwamba lengo kubwa serikali ni kuweka mikakati madhubuti ambayo itawasaidia kuwakomboa wakulima wa zao la muhogo hivyo ujenzi wa kiwanda hicho utakuwa ni mkombozi mkubwa na chachu ya kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo.
Aidha, Ndikilo amewataka maofisa ugani waliopo Mkoani humo kujenga tabia ya kuwatembelea wakulima wa zao la muhogo ili waweze kutoa elimu ya namna ya uzalishaji wa zao hilo.
Alisema ,zao la Muhogo ni moja ya zao muhimu na kwamba likitumika vizuri linaweza kuwaongezea wakulima kipato na hata kuongeza kipato cha Mkoa na hata kujenga uchumi wa Taifa.
Ndikilo ,alisema kuwa wakulima wengi wanalima zao hilo huku wakiwa hawana utaalamu wala elimu ya kutosha juu ya zao hilo na kwamba ni wakati wa maafisa ugani kuona namna ya kuwatembelea wakulima kwa kuwapa elimu ya zao hilo.
Aliongeza kuwa,mkoa wa Pwani unajumla ya hekta 3,353,900 ambapo eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 1,933,224 sawa na asilimia 57.66 ya eneo lote.
Alisema, pamoja na kuwepo kwa ukubwa wa eneo hilo lakini bado Muhogo hulimwa kwa kiasi kidogo ikiwa ni wastani wa hekta 60,703 na kuzalisha tani 500,000 hadi 650,000 kwa mwaka huku akisema eneo hilo ni asilimia tatu.
" Kwa upande wa tija nayo ipo chini kwa miaka mitano iliyopita uzalishaji kwa eneo ni wastani wa tani 6.5 hadi 7.6 kwa hekta ingawa yapo maeneo machache hasa Kibiti na Rufiji ambako tija ni kati ya tani 9 hadi 18 kwa hekta wakati tija inayopendekezwa kitaalamu kuwa ni tani 20 kwa hekta" alisema Ndikilo.
Kuhsu usindikaji mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa bado haufanyi vizuri pamoja na kuwepo kwa juhudi za kuanzisha vikundi na Viwanda vya usindikaji kwani vikundi 32 vilivyopo katika Mkoa huo havisindiki mihogo kwa madai ya kukosa soko la uhakika.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wadau wa Zao la Muhogo (TACAPPA) Mwantumu Mahiza, alisema endapo wakulima watahamasishwa kuhusiana na zao hilo litawasaidia kujikwamua kutoka kwenye umasikini.
Mahiza, alisema maaofisa ugani wanatakiwa kusaidia kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kulima zao hilo kitaalamu na kupata mbegu bora na kwamba bila hivyo hakuna mafanikio yatakayopatika.
Alisema,chama hicho kimejipanga kupambana na vikwazo vya soko la zao hilo ambapo vikitolewa wakulima watachangia kuinua uchumi wa taifa na kuondoa umasikini wa kaya.
Mahiza,alisema kuwa kwasasa Taccapa kipo katika mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha Muhogo ambacho kitahudumia Mikoa ya Kanda ya Mashariki na Kati na kufanya Muhogo kupata soko kubwa zaidi.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Dkt.Dolphine Magere,alisema kuwa kikao hicho kinalenga kutoa dira ya kuhakikisha zao Muhogo linapata hadhi kama mazao mengine.
Magere,alisema baada ya kikao hicho timu mbalimbali kupitia Halmashauri zitaundwa kwa kuwashirikisha maafisa ugani ili kusudi wawe karibu na wakulima wa zao hilo.
.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.