Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amesema ujenzi wa kiwanda cha dawa muhimu za binadamu cha M-Pharmaceuticals Ltd ni utekelezaji kwa vitendo wa agizo la Rais John Magufuli la kujenga viwanda vya dawa hapa nchini.
Mhandisi Ndikilo ameyasema hayo wakati akitoa salam za Mkoa katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha dawa cha M-Pharmaceuticals ambacho kinatarajiwa kujengwa wilayani Bagamoyo.
Ndikilo amesema kuwa kwa Mkoa wa Pwani kiwanda cha M -Pharmaceuticals kinaungana na viwanda vingine vitatu vya dawa za binadamu vitakavyojengwa Mkoani hapa na hivyo kuufanya Mkoa kuwa na viwanda vinne.
Pia Mhandisi Ndikilo amevitaja viwanda hivyo vingine ikiwa ni pamoja na Zinga Pharmaceuticals Ltd kitakachojengwa eneo la Zinga Bagamoyo, Kairuki Pharmaceuticals Ltd na Bahari Pharmaceuticals Ltd vitakavyojengwa eneo la Zegereni mjini Kibaha.
"Nawapongeza sana kampuni ya M-Pharmaceuticals Ltd chini ya uongozi wa Dk Mengi na mbia mwenzake Dk Nagesh Bhandari kutoka nchini India kwa kuamua kujenga kiwanda hiki cha madawa muhimu kwa ajili ya binadamu hapa Kerege, maana hatua hii mliyoichukua ni kuunga mkono juhudi za Mkoa wa Pwani za kuendeleza ujenzi wa viwanda,"amesema Ndikilo.
Ndikilo amebainisha kuwa uamuzi wao huo na ule wa wawekezaji wa sekta nyingine unauweka Mkoa wa Pwani kwenye nafasi nzuri katika ramani ya uwekezaji wa Viwanda hapa nchini na hivyo kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa Viwanda.
Ujenzi wa Kiwanda cha M-Pharmaceuticals unatarajia kumalizika baada ya miezi 18 na uzalishaji wake unatarajia kuanza pindi tu kitakapomalizika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.