Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani imeendesha kongamano maalum la kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha, kugombea, na kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Kongamano hilo limefanyika Oktoba 9, mjini Kibaha, likihusisha makundi mbalimbali kama vile vyama vya siasa, viongozi wa dini, wasanii, bodaboda, mamalishe, machinga, mashirika yasiyo ya kiserikali, na mengineyo.
Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchata, amesema kuwa kongamano hilo ni sehemu ya maandalizi ya kufanikisha uchaguzi huo.
Mchata alisisitiza umuhimu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwa unapeleka madaraka kwa wananchi, hasa kupitia wenyeviti wa serikali za mitaa na vitongoji ambao huchaguliwa moja kwa moja na wananchi.
Aliongeza kuwa Mkoa wa Pwani umejipanga vizuri na unaratibu shughuli zote za uchaguzi, huku akitoa wito kwa makundi hayo kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha, kugombea, na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Pia aliwasisitiza kutumia kanuni za “4R” za Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na bila migogoro.
Mchata aliwakumbusha wawakilishi wa makundi hayo kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, ambapo zoezi hilo litaanza Oktoba 11 na kumalizika Oktoba 20, mkoani Pwani.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Mkoa wa Pwani, George Nsajigwa, alieleza kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri, na kongamano hilo lililenga kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu.
Nsajigwa alibainisha kuwa Novemba 1 hadi 7 itakuwa ni kipindi cha uchukuaji wa fomu, kampeni zitaanza Novemba 20 hadi 26, na Novemba 27 ni siku rasmi ya kupiga kura.
John Kirumbi, Mwenyekiti wa Wazee Wastaafu wa Mkoa wa Pwani, aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuandaa kongamano hilo, akibainisha kuwa litasaidia kuongeza hamasa ya wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.