Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameiagiza Halmashauri ya wilaya ya Kisarawe kuhakikisha ujenzi wa mradi wa shule ya Sekondari ya Kitanga iliyopo kata ya Msimu unakamilika kabla ya Novemba 23 mwaka huu.
Ametoa maagizo hayo leo Novemba 9, 2023 alipozungumza na wanachi wa Kitanga mara baada ya ukaguzi wa mradi wa shule hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Mkoani humo.
Amesema hatua hiyo itasaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kufuata huduma ya elimu umbali mrefu na akaielekeza TANESCO kufikisha Nishati ya umeme katika shule hiyo ifikapo Disemba 15, 2023.
Aidha ameielekeza Wakala wa maji na Vijijini RUWASA kuangalia namna ya kufikisha maji shuleni hapo ili wanafunzi wapate maji safi na Salama na kuwa huduma hizo za umeme na maji zitanufaisha shule pamoja na wananchi wa eneo hilo.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wazazi kuwapa fursa watoto wa kike ya kupata elimu akisema "Ninasisitiza Elimu kwa Watoto wa kike izingatiwe, kama tunataka hamsini kwa hamsini ni lazima watoto wa kike wasomeshwe, kutokana na hilo ndio maana Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kujengwa shule, Mabweni kwa ajili ya watoto wa kike."
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Fatma Nyangasa amesama, kata ya Msimbu ilikuwa na Shule moja ya Sekondari hali ambayo ilisababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya Sekondari.
Katika ziara hiyo Mkuu huyo wa Mkoa pia ametembelea ujenzi wa chuo cha ufundi VETA, akakagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri, kisha kuongea na wananchi katika Mkutano wa hadhara ambako alisikiliza, kutoa ufafanuzi na kutatua kero na malalamiko yaliyowasilishwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.