Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge amezihamasisha halmashauri za mkoa huo kuanzisha redio za kijamii ili kuweza kutoa taarifa zitakazosaidia kutatua changamoto katika jamii kwa kuhabarisha, kuburudusha na kutoa elimu juu ya mambo yanayofanywa na Serikali na yale yanayopaswa kuzingatiwa na wananchi pamoja.
Kunenge aliyasema hayo Aprili 29, 2023 alipotembelea na kukagua Kituo cha Redio cha Chalinze FM 97.5 "Sauti ya Jamii" ambacho kimeanzishwa kwa gharama zilizopatikana kupitia mapato ya ndani ya Halmshauri ya Wilaya ya Chalinze.
Kunenge amepongeza jitihada ya Halmashauri hiyo kuweza kuanzisha Mradi huo ambao ni wa kwanza katika mkoa wa Pwani na kuwa kituo hicho kinasikika katika Wilaya yote ya Bagamoyo na maeneo mengine ya jirani kupitia mawimbi ya 97.5 FM.
"Kituo hiki ni kizuri na cha kisasa, Wananchi wanaweza kupata taarifa, kujua juu ya mambo yanayofanywa na serikali pamoja na chama tawala na hasa katika masuala ya kiafya, elimu, utunzaji mazingira, kuboresha maadili kwa vijana na watoto kwani kwa sasa kuna changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili yanayofanyika," alisema Kunenge.
Aliongeza kuwa kwa kutumia redio hiyo serikali itaweza kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimaendeleo na akaelekeza kuandaliwa vipindi vyenye maudhui yenye maadili sahihi tofauti na yale yanayopotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari na akasisitiza kuwa kwa kutumia kituo hicho wananchi wataweza kusikiliza, kujifunza na kupata taarifa sahihi juu ya mambo yanayozingatia maadili ya nchi ya Tanzania na ya dini za watanzania.
"Tuzingatie kuwa na vipindi vizuri ambavyo vitasaidia kutatua changamoto katika jamii kwa maana ya kuhabarisha serikali inafanya nini na kutoa elimu kuhusu mambo gani wanapaswa kuzingatia, kituo hiki pia kiweze kuburudisha baada ya kazi za kulitumikia taifa, kazi za kijamii na za kiuchumi." aliongeza Kunenge.
Aliongeza kuwa pamoja na mambo hayo, uanzishwaji wa redio hiyo pia utasaidia kutoa ajira kwa vijana na akatoa rai kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji Mkoani humo kutumia Kituo hicho kutangaza bidhaa wanazozalisha au huduma wanazotoa.
Katika hatua nyingine, akiwa kituoni hapo, Mhe. Kunenge pia alitoa taarifa kuwa Mkoa wa Pwani unatarajia kuupokea mwenge wa Uhuru Mei 15, 2023 ukitokea Mkoani Morogoro na utakimbizwa katika Wilaya zote saba na hamalashauri tisa kisha utakabidhiwa Mkoani Dar es Salaam Mei 24, 2023, hivyo akawaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mapokezi hayo na kwenye maeneo yote utakakopitishwa kukagua, kuweka mawe ya msingi au kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mbali na mradi huo, Mhe. Kunenge pia alikagua mradi wa stendi ya magari ya abiria chalinze, pia akafika na kukakagua ujenzi wa mradi wa barabara, nyumba za watumishi wa afya na taa za barabarani katika mji wa Bagamoyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.