MKuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,amekutana na wananchi wa Wilayani Bagamoyo kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi hususani migogoro ya ardhi.
Kunenge,amefika Wilayani Bagamoyo Januri 24 ikiwa ni sehemu ya kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa (MB)aliyoitoa mwishoni mwa wiki iliyopita Wilayani Bagamoyo.
Mchengerwa,alitoa maagizo hayo katika ziara ya Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Paul Makonda ambaye alipita Wilayani humo na kupokea changamoto mbalimbali ikiwemo masuala ya Ardhi.
Akiwa Wilayani Bagamoyo Kunenge amekutana na wananchi mbalimbali ambapo mbali na kutatua kero hizo amezungumza na Wananchi hao huku akisema Serikali ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ni sikivu.
Kunenge,amesema Serikali lazima ihakikishe kila mwenye haki anapata haki yake bila kuonea mtu na kikubwa ni ukweli kwakuwa ukweli unamuweka mtu huru.
"Nimekuja hapa kusikiliza kero na changamoto zenu lakini lazima tujue yapo ambayo yatapata majibu hapa hapa na mengine kutoka nayo kwenda kuyafanyiakazi na ambayo yatakuwa juu ya uwezo wetu tutayapeleka juu,"amesema Kunenge
Awali akimkalibisha Mkuu wa Mkoa , mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Halima Okash alisema kuwa tayari walishaanza kushughulikia migogoro ya hiyo kwa kuanzisha clinic ya ardhi kama walivyoelekezwa na kata zote 20 za Wilaya ya bagamoyo zilitembelea na waliweza kutataua migogoro kwa asilimia 80 na mingine iliyosalia bado ipo katika hatua mbalimbali za kimahakama.
Kwa upande wa wananchi wamemshukuru Mkuu wa mkoa kwa ujio wake na wamemuomba aendelee kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinzowakabili wananchi ili kuboresha maisha yao.
Katika ziara hiyo Kunenge ameambatana na wataalamu kutoka ofisini kwake ikiwemo kitengo cha idara ya ardhi na Sheria pamoja kamati ya ulinzi na usalama ya Wilayani Bagamoyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.