Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amelitaka jeshi la Polisi Wilayani Bagamoyo kumchukulia hatua za kisheria Hassan Usinga "Wembe" kwa tuhuma za kumdhalilisha aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo na Waziri wa Miundombinu Dk Shukuru Kawambwa.
Kunenge ameyasema hayo wakati wa kikao baina ya Dk Kawambwa na Wembe na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Bagamoyo akiwemo Mkuu wa Wilaya Halima Okash na Mkurugenzi wa Halmashauri Shauri Selenda na baadhi ya wakuu wa idara mbalimbali.
Alisema kuwa suala hilo limesababisha kuhatarisha usalama wa Mkoa na taharuki kwa baadhi ya watu nchini kutokana na kitendo hicho cha udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kufungwa pingu kwa kiongozi huyo mstaafu ambapo serikali haikubaliani nacho.
"Mwekezaji wa machimbo hayo ya mchanga ana vibali vyote vya umiliki na uchimbaji lakini changamoto iliyotokeza ni uharibufu wa barabara uliofanywa na malori ya yanayopita hapo yanayobeba mchanga na kuharibu barabara kutokana na uzito mkubwa na kusababisha wananchi kuifunga,"alisema Kunenge.
Naye Dk Kawambwa alisema kuwa alifungwa pingu na mtuhumiwa huyo akishirikiana na mgambo Abdala Mgeni na kusukumwa hali ambayo ilimfanya ajisikie vibaya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okash alisema kuwa mwekezaji aliomba kibali cha shughuli za uchimbaji mchanga na baraza la madiwani likamkubalia baada ya kufuata taratibu zote kuanzia ngazi ya chini.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile alisema kuwa walizuia kutumika barabara hiyo ilifungwa kutokana na kuharibika lakini bado iliendelea kutumika kupitisha malori ya mchanga ambapo inauwezo wa kutumika na malori yenye uzito wa tani 10.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.