Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa muda wa wiki mbili kwa mkandarasi Elray, anayejenga jengo la kisasa la maduka makubwa (shopping mall) lililopo Halmashauri ya Mji Kibaha, kukamilisha ili wafanyabishara waanze kuuza bidhaa zao.
Ujenzi wa jengo hilo ambalo ni mradi wa Halmashauri ya Mji Kibaha umefikia asimilia 98, kinachosubiriwa kwa sasa ni kukamilisha baadhi ya miundombinu ili lianze kutoa huduma.
Kunenge ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 25, 2023 kwenye ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo soko, barabara na shule ambapo amesema ameridhishwa na kasi ya ukamilishaji wa miundombinu hiyo.
Amesema kukamilika kwa jengo hilo la kisasa kutatoa fursa kwa wafanyabiashara 253 kuuza bidhaa zao.
“Mradi huu wa maduka makubwa una manufaa makubwa sana na tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kujenga tutazalisha ajira na fursa nyingi za uwezeshaji wananchi kiuchumi,” amesema Kunenge.
Katika hatua nyingine Kunenge, ametoa kibali kwa wafanya biashara wadogo "wamachinga" kujenga miundombinu ili kufanya biashara kwenye eneo ambalo awali liliwekwa kwa ajili ya matumizi mengine kwa madai kuwa kufanya hivyo kutatoa fursa kwa wananchi kupata huduma wanazozitaka kwa wakati mmoja.
Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Brighton Kisheo amesema mwaka 2018/2019, halmashauri hiyo ilitengewa kiasi cha sh. bilioni nane kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Amesema baada ya kukamilika kwa mradi huo, wanatarajia kuingiza kiasi cha sh. milioni 450 kwa mwaka fedha ambayo itatokana na uendeshaji wa jengo hilo la maduka makubwa (Shopping Mall) la Halmashauri ya Mji Kibaha.
Naye mwenyekiti wa Wamachinga mkoa wa Pwani Filemon Maliga amemshuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia eneo jirani na jengo hilo ili wafanye biashara zao na akaeleza kuwa wanaona fahari kundi la wamachinga kutambulika na kupata fursa mbalimbali zikiwemo za mikopo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.