Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameziagiza halmashauri mkoani humo, kuhakikisha zinatoa fedha kwa wakati katika kutekeleza masuala ya lishe.
Aidha amekemea vikali tabia ya baadhi ya Halmashauri kutenga fedha za kutekeleza shughuli nyingine kupitia vifungu vinavyohusisha masuala ya lishe hali inayosababisha utekelezaji wa shughuli za lishe kushindwa kufanyika kwa wakati.
Kunenge ameeleza hayo Mei 14 wakati akifungua kikao cha nusu mwaka cha Tathmin ya mkataba wa lishe, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Destiny, mjini Kibaha ,kilichowajumuisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na maafisa lishe ngazi ya mkoa na Halmashauri.
"Mh. Rais amesaini mkataba wa lishe na Wakuu wa Mikoa na kutoa fedha kisha anatokea mtu anaenda kufanya vile anavyotaka yeye kwa kuweka fedha za shughuli nyingine kwenye vifungu vya masuala ya lishe hili jambo liachwe mara moja " amesema Kunenge.
Ameeleza, kifungu kimewekwa kwa malengo ya shughuli ya lishe , ifanye masuala ya lishe peke yake na si vinginevyo .
Kadhalika Kunenge amezipongeza halmashauri za Kibaha na Halmashauri ya Wilaya kibaha, kwa kufanya vizuri katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa mwaka 2022/2023 ambapo mkoa wa Pwani ulishika nafasi ya kwanza kitaifa.
Kunenge ameeleza kuwa, Serikali chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada za kuhakikisha kila Halmashauri inapata Afisa lishe zaidi ya mmoja ",hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wa mkataba huo katika ngazi zote"
"Niwahimize viongozi wenzangu kusimamia lishe kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa kata kwani utekelezaji wake unalenga kuifikia jamii" anasema Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.