Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezielekeza Halmashauri za Mkoa huo kuibua vyanzo vipya vya mapato na kuongeza umahiri wa kukusanya sambamba na kuwa makini kwenye matumizi kwa kutumia maeneo yenye tija.
Kunenge ameyasema hayo kwa nyakati tofauti leo Juni 20, 2024 alipohudhuria vikao vya mabaraza ya Halmashauri ya Mkuranga na Kisarawe kujadili hoja za Ukaguzi wa Hesabu za Serikali katika maeneo hayo.
Amezileza Halmashauri hizo kuwa Mapato yanatengenezwa, hivyo ni lazima waweke mikakati ya kuibua vyanzo vipya na kuvifanya vikue na kuwa endelevu katika kuongeza mapato ya Halmashauri.
"Fursa mnazo na mnafanya vizuri lakini mnaweza kufanya vizuri zaidi ya hapo, kinachotakiwa sio tu asilimia ya makusanyo ya lengo (bajeti), bali ni kiasi gani unapata ili kuwaletea wananchi maendeleo," amesema.
Amewasisitiza madiwani na watendaji katika halmashauri hizo kuwa wakati wote wafikirie nini wanaweza kufanya ili kuzisaidia halmashauri zao kutoa huduma kwa wananchi.
"Jifunzeni, kuweni wabunifu na uzeni fursa zenu ili ziweze kuzalisha na kuwapatia tija, tumieni vizuri fursa zote," amesisitiza.
Akiongelea matokeo, Mkuu huyo wa mkoa ameziasa halmashauri hizo kutekeleza mradi mmoja kwa ukamilifu ndipo watekeleze mradi mwingine badala ya kugawa fedha kidogo kidogo kwa miradi ambayo matokeo yake ni kutokamilika na kutoleta tija kwa jamii akisema "Mnagawana vifedha vidogo vidogo vya ujenzi wa barabara matokeo yake hakuna kitu kinachoeleweka katika miradi hiyo."
Katibu Tawala wa Mkoa huo ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchatta amezipongeza Halmashauri hizo kwa kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir ametoa Rai kwa watumishi kuwa waadilifu na kila Mkuu wa idara anatakiwa kukaa na wataalamu wake na kujadili mikakati ya kuinua mapato.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti amemuahidi Mkuu wa Mkoa huo kushirikiana na Watendaji kuzuia uzalishaji wa hoja mpya sambamba na kusimamia utekelezaji wa miradi iliyoelekwzwa katika Wilaya hiyo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.