Wakala wa Barabara Mkoani wa Pwani (TANROADS) imesema ongezeko la shughuli za kilimo kandokando ya mito hususani ndani ya mto Rufiji zinachangia kuzuia maji kupita na kukusanya mchanga katikati ya daraja hali ambayo inaweza kusababisha hatari ya kukatika kwa barabara wakati wa mvua.
Hayo yameelezwa katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani kilichofanyika jana mjini Kibaha na kuwahusisha Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo, wakurugenzi na wahandisi kutoka TANROADS na TARURA.
Akitoa taarifa ya mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2020/2021 wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani (TANROADS) bi. Christina Nyamziga ambaye ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango aliainisha changamoto hiyo kuwa imekuwa kikwazo kwa barabara kudumu kwa muda mrefu bila matengenezo.
Bi. Nyamziga alisema mbali ya kilimo pia ipo changamoto ya wizi wa samani za barabara, ongezeko la mifugo kwa baadhi ya maeneo ya Mkoa huo pamoja na upatikanaji wa changarawe inayofaa kwa ujenzi.
"Changamoto nyingine ni kutopatikana kirahisi mtaalam wa matengenezo ya mizani ya Vigwaza inayopima magari yakiwa yanatembea, wakati mwingine ikitokea uharibifu katika mzani magari yote huingia kupima kwenye mzani mmoja hali ambayo husababisha foleni na usumbufu kwa watumiaji wa barabara" alisema.
Bi Nyamziga aliwasilisha taarifa ya mapendekezo ya shilingi milioni 973.820 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara kutengeneza kilomita 16.40, na shilingi bilioni 1.75 kugharamia miradi ya Serikali Kuu kwa kutengeneza kilomita 25 za barabara za Mkoa.
Alibainisha kuwa kiasi cha shilingi bilioni 4, 94 kimelenga kugharamia miradi ya Serikali Kuu kwa kujenga kilomita 5.7 za barabara kuu.
Nyamziga alisema, katika bajeti ya mwaka 2019/2020, jumla ya shilingi bilioni 22.47 zilipangwa kutumika katika matengenezo mbalimbali ya barabara.
Alisema hadi kufikia mwezi Desemba shilingi bilioni 8.697 zilipokelewa kwa ajili ya matengenezo ya barabara mbalimbali, ambapo Shilingi bilioni 3.424 zimetumika kufanya matengenezo ya barabara kuu na za Mkoa.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alitoa rai kwa Wakala wa Barabara Mkoa wa Pwani na Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini kuhakikisha wanasimamia barabara ziendane na thamani ya fedha zinazotolewa.
Aidha Amewataka wakala hao TANROAD na TARURA Mkoa wa Pwani kushirikiana na viongozi wa Vijiji ,Kata,Tarafa na Wilaya katika kulinda miundombinu na kufahamu hali ya Barabara wanazoudumia katika pindi hiki cha Mvua.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.