Wakala wa barabara Mkoa wa Pwani unatarajia kutumia kiasi cha shilingi billion 25.4 kwa ajili ya kufanya matengenezo mbalimbali ya barabara.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mhandisi Zuhura Aman wakati wa kikao cha bodi ya barabara Mkoani Pwani na kusema kuwa fedha hizo ni bajeti ya mwaka 2018/2019.
Pia alisema kuwa hadi kufikia Septemba 2018 shilingi milioni 958.7 zimepokelewa ajili ya matengenezo mbalimbali.
“Mkoa umepanga kutekeleza miradi ya maendeleo ya barabara zenye urefu wa kilometa 32.5 zenye thamani ya shilingi bilioni 2.3”alisema Mhandisi Aman.
Aidha alisema kuwa ili kutekeleza miradi ya barabara; shilingi bilioni 1.3 zimetengwa katika bajeti ya Wakala wa Barabara, shilingi milioni 969 kutoka mfuko wa Barabara na shilingi bilioni 7.5 ni kutoka Serikali Kuu. Fedha hizo zitatumika kufanya ukarabati wa barabara kwa kiwango cha changarawe/udongo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa ili kuweza kuboresha Barabara za Mkoa huo watendaji wanapaswa kuwa waadilifu katika utendaji wao wa Kazi.
Ndikilo alisema kuwa kutokana na Mkoa kuwa na Viwanda vingi uboreshaji wa miundo mbinu ya barabara ni muhimu sana na utasaidia kuinua uchumi wa wananchi Pwani na taifa kwa ujumla
.”Muwe makini na baadhi ya watu wanaoharibu na kuhujumu miundombinu ya barabara zetu ikiwemo baadhi ya watu wanaozidisha uzito na kuiba alama za barabarani”alisema Ndikilo.
Katika Hatua nyingine Mhandisi Ndikilo amempongeza Mhe Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa ujenzi wa barabara nane, utakaoanzia Kimara hadi Tamco - Kibaha. Aidha amempongeza kwa kutenga shilingi bilioni 65 kwa ajili ya upanuzi wa daraja la Mto Wami.
“Pamoja na pongezi hizo pia tutapeleka ombi moja tu kupita TANRODS kuwa njia hizo nane zisiishie TAMCO bali zifike hadi kwa Matiath kwani ndipo kitovu chetu cha mji kilipoanzia”alisema Mhandisi Ndikilo.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas Msangi alisema kuwa changamoto zote ambazo zimetolewa na wajumbe wa bodi ya barabara zitafanyiwa kazi kulingana uwezo wa kibajeti.
Mhandisi Msangi alisema kuwa malengo yao ni kuhakikisha barabara zinajengwa kwa kiwango kinachostahili ili ziweze kupitika kwa wakati wote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.