Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema lishe bora ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa na kusisitiza kuwa haiwezekani kujenga uchumi imara bila wananchi wenye afya njema.
Ametaka mpango wa lishe kutekelezwa kwa ufanisi, kwani fedha zinazotolewa kwa ajili hiyo ni uwekezaji kwa ustawi wa jamii na vizazi vijavyo.
Akihitimisha kikao cha lishe cha Mkoa wa Pwani kilichofanyika Septemba 9, 2025, Kunenge alisema Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha suala la lishe linawekwa kwenye ajenda kuu za maendeleo.
"Mpango huu unapaswa kuendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inalenga kujenga wananchi wenye uwezo na tija katika maendeleo," amesema.
Aidha, RC Kunenge alihimiza wataalamu na watendaji wa sekta husika kusimamia kwa karibu utekelezaji wa afua za lishe, ili kuhakikisha Mkoa huo unaendelea kushika nafasi ya kwanza kitaifa.
"Msisitizo huu unatakiwa kuungwa mkono na mipango ya halmashauri pamoja na ushirikiano wa wananchi," amehimiza.
Katika hatua nyingine, Kunenge amewataka wananchi wa Mkoa wa Pwani kuendelea kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara.
Amesema hatua ya kujitambua kiafya mapema ni njia bora ya kuzuia changamoto kubwa zinazoweza kuathiri ustawi wa jamii.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, alisema ni muhimu mpango wa lishe ukabidhiwe sura inayozingatia mahitaji halisi ya jamii na akasema kuwa kwa kufanya hivyo, Mkoa utakuwa na nafasi ya kuimarisha afya ya wananchi na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.