Maafisa Habari wawili kutoka Mkoa wa Pwani wameshiriki katika warsha ya siku tano ya mafunzo ya mawasiliano ya kimkakati yaliyoandaliwa kupitia Programu ya Shule Bora. Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Korogwe Executive, wilayani Korogwe, mkoani Tanga, yakiwa na lengo la kuwajengea washiriki uwezo wa kitaalamu na kiufundi katika nyanja ya mawasiliano ya maendeleo.
Warsha hiyo imefunguliwa rasmi na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uratibu na Mipango Mkoani humo Amina Kibunde, aliyesisitiza umuhimu wa Maafisa Habari wa Serikali na taasisi kuimarisha jitihada za uhamasishaji na utoaji wa taarifa kuhusu miradi ya maendeleo, hasa ile inayotekelezwa katika sekta ya elimu.
“Mafunzo haya yamekusudiwa kuwajengea uwezo wa kiufundi Maafisa Habari katika kuandaa na kusambaza maudhui yanayoonyesha mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya elimu nchini kwani Serikali imefanya mambo makubwa na mazuri hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha wananchi wanayafahamu kupitia mawasiliano yenye tija,” alisema Amina.
Ameongeza kuwa kuna haja ya kutumia mifumo mbalimbali ya mawasiliano kueneza taarifa za miradi ya serikali ili kuunga mkono juhudi za maendeleo, huku akiwataka Maafisa Habari kuhakikisha maudhui wanayoyaandaa yana manufaa, yanaongeza uelewa kwa wananchi na kuchochea ushiriki wao katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Programu ya Shule Bora, Bi. Virginie Briand, alibainisha kuwa warsha hiyo inalenga kusaidia Maafisa Habari kuwasilisha mafanikio ya Programu ya Shule Bora, na kuwawezesha kushiriki katika kuandaa mpango mkakati wa mawasiliano unaolenga kuendeleza mafanikio ya programu hiyo hata baada ya kufikia ukomo wake.
Katika siku ya kwanza ya mafunzo, washiriki walipata nafasi ya kujifunza mada mbalimbali ikiwemo muhtasari wa Programu ya Shule Bora (Shule Bora Overview), misingi ya mawasiliano ya kimkakati, uandaaji wa mikakati ya mawasiliano, na mbinu za kujenga uwezo wa kitaaluma katika kuwasilisha taarifa zenye athari chanya kwa jamii.
Mafunzo hayo yamewakutanisha Maafisa Habari wa Serikali kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi za elimu zinazofanya kazi na Shule Bora, pamoja na Maafisa Habari kutoka Mikoa tisa ambayo ni Dodoma, Simiyu, Mara, Singida, Kigoma, Katavi, Rukwa, Tanga na Pwani
Kwa upande wa Mkoa wa Pwani, washiriki wa warsha hiyo ni Zablon Bugingo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, na Hidaya Hadoswa, Afisa Habari Daraja la Pili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.