Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ally, leo Agosti 4, 2025, ametembelea Banda la Halmashauri ya Wilaya ya Mafia katika Maonesho ya Nanenane ya Kanda ya Mashariki yanayofanyika Morogoro, ambapo ametoa wito kwa wananchi, hususan wazee na wafanyabiashara wadogo, kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa lengo la kukuza mitaji na kuimarisha biashara zao.
Dkt. Mussa amesisitiza umuhimu wa viongozi wa halmashauri kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu na fursa za upatikanaji wa mikopo hiyo isiyo na riba, ili kuhakikisha inawanufaisha walengwa wengi zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia, Shabani Shabani, amethibitisha upatikanaji wa mikopo hiyo na kuwahimiza wananchi kujitokeza kuomba akibainisha kuwa mikopo hiyo haina riba kabisa na masharti yake ni nafuu.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa sera zake bora zinazoendeleza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa mwaka 2025 ili kuchagua viongozi bora watakaosukuma mbele maendeleo ya sekta hizo, sambamba na kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu inavyosema Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.