Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza wakuu wa wilaya nchini kushirikiana na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kusimamia na kukagua wa mashine za EFD ili kuepusha upotevu wa fedha za Serikali.
Akifunga wiki ya Utalii na Uchumi wa bluu Wilayani Mafia, Majaliwa ameelekeza wakuu wa wilaya pia kusimamia na kuimarisha mabaraza ya biashara kwenye maeneo yao ili suala la biashara lilete tija kwa wafanyabiashara na kupata faida.
"Nyie wakuu wa wilaya ni wenyeviti wa mabaraza haya, kaeni kwenye vikao vya mapato kwenye maeneo yenu, fanyeni ukaguzi ili kubaini kama mitambo ya EFD ni halisi kwani baadhi zinapoteza mapato ya Serikali na kuleta usumbufu kwa wananchi," amesema Majaliwa.
Akizungumzia uchumi wa Mafia, Majaliwa ameelekeza wilaya hiyo na mkoa wa Pwani kuendelea kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika uchumi wa bluu kisiwani humo ili kujiongezea mapato na kukuza uchumi.
Vilevile Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri katika Kisiwa hicho ambapo imetenga shilingi Bilioni 9.5 ya kutengeneza kivuko kingine chenye uwezo wa kubeba tani 120 ya mizigo na abiria 500.
Ameupongeza mkoa wa Pwani na wilaya ya Mafia kwa kufanikisha tamasha hilo na kutangaza vivutio na akawashauri lisiishie hewani liwe bali liwe endelevu kwa kila mwezi Septemba ya kila mwaka.
Waziri Mkuu huyo ameeleza kuwa Mafia ni kisiwa ambacho kinasifika kwa mazalia ya samaki Duniani na kuwa kisiwa hicho kinachangia pato kubwa kupitia Uchumi wa bluu na Uvuvi.
Nae Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Abubakari Kunenge, alieleza kuwa tamasha hilo limefanyika kwa siku tatu lilianza Septemba 28 hadi leo Septemba 30 ambapo washiriki walikuwa 71.
"Hili tunalofanya ni kutafsiri kwa vitendo azma ya Rais kufungua wilaya ya Mafia katika uwekezaji wa uchumi wa bluu na utalii na kwa hili tukio, imani yetu mwaka mmoja matokeo chanya yataonekana "amesema Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.