Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suhulu Hassani ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani kushirikiana na vyombo vya usalama kulinda amani na usalama wa Mkoa wa Pwani kufuatia kujitokeza kwa mambo ambayo yameonekana kuhatarisha usalama mkoani hapa. Rai hiyo imetolewa na Mhe. Makamu wa Rais wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Chalinze Wilayani Bagamoyo na Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wakati akiwa njiani kuelekea Mkoani Dodoma
Akiwa katika Eneo la Mlandizi kibaha,
Mhe. Makamu wa Rais ameahidi kuweka uzio wa katika kituo cha Afya cha Mlandizi ambapo itakuwa ni moja ya sifa ya kupandishwa hadhi ya kuwa Hospitali ya Wilaya kwani serikali bado ina nia ya kupandisha hadhi vituo mbalimbali na kuhakikisha uwepo wa dawa katika kituo cha Afya cha Mlandizi.Kuhusu kupimwa kwa Mji wa Mlandizi Mhe. Makamu wa Rais ameahidi atafanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi ili waweze kupima eneo hilo na suala la barabara ya Makofia Mzenga amesema ahadi iko palepale kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami.Pia ameongezea kwamba kuhusu eneo la Kisabi A na B ambalo limepimwa na limezuiliwa na TAMISEMI, Mhe. Makamu wa Rais ameahidi kwamba atafanya mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili waweze kuyaachia maeneo hayo.
Akiwa Chalinze Wilayani Bagamoyo, Mhe. Makamu wa Rais amewahakikishia wananchi wa chalinze kutatua tatizo la maji katika mji wa Chalinze na kuhusu mradi wa maji Chalinze upo katika hatua za mwisho na Serikali imeandaa mpango mzuri wa kupunguza tatizo hilo la maji katika Mji wa Chalinze.Amesema upo mpango wa kuvuta maji kutoka mto Wami mpaka Pera kwa mabomba na kujenga matanki makubwa ili maji yakifungwa yaweze kuwafikia Wananchi kwa urahisi.
Pia ameongezea kuwa Serikali inampango wa kujenga Tanki jingine la kuhifadhia maji maeneo ya Mazizi yenye lita za ujazo milioni 1.2 ambalo litawawezesha wakazi wa Chalinze kutumia maji kwa wiki mbili bila kukatika .
Aidha ameongezea kuwa vifaa vya tiba vipo katika Hospitali ya Msoga ila tatizo ilikuwa ni mafundi wa kufunga vifaa hivyo, ataiagiza Wizara ya Afya kupeleka wataalam kwa ajili ya kufunga vifaa hivyo na amesema kuwa na kituo cha Afya cha Chalinze bado suala lake linashughulikiwa.
Hata hivyo Mhe. Makamu wa Rais amemuagiza Mkuu wa Mkoa Pwani kuwa mpaka ifikapo mwezi Novemba awe tayari amempatia taarifa ya tathmini ya eneo la soko la Chalinze. Pia amewataka wakulima na wafugaji kuacha migogoro na amewaagiza viongozi wa Wilaya kusimamia ipasavyo suala la Migogoro ya wakulima na wafugaji
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.