Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeanza kutoa mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa maafisa waandikishaji wa Mkoa wa Pwani walioteuliwa kwa ajili ya kusimamia zoezi hilo
Mafunzo hayo yameanza kutolewa leo katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani zilizopo Mjini Kibaha yakiwajumuisha maafisa waandikishaji,maafisa waandikishaji wasaidizi,maafisa uchaguzi,na maafisa Tehama wa Halmashauri za Mkoa.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Kamishina wa Tume ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji mstaafu wa Mahakama kuu Mary Longway,alisema kuwa zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.
Alisema kuwa,mafunzo hayo yanatolewa kwa awamu tatu na kwamba awamu ya kwanza ni kwa ajili ya ngazi ya Mkoa ,ngazi ya Jimbo na baadae ngazi ya Kata huku lengo kubwa ni kuhakikisha kila mwananchi anajiandikisha.
"Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura ni endelevu kwakuwa tayari limepita Mikoa mingi hapa nchini na sasa tupo Pwani kwahiyo Tume imejipanga vizuri kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kujiandikisha,"alisema Longway.
Kwa upande wake mratibu wa uandikishaji Mkoa wa Pwani Gerald Mbosoli, alisema kuwa baada ya kumaliza mafunzo hayo kwa maafisa waandikishaji hatua itakayofuata ni kuingia katika Mitaa kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo.
Mbosoli,alisema zoezi la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura litaanza rasmi Februari 14 na kumalizika Februari 20 mwaka huu na kwamba Tume imetoa siku Saba kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo.
Aidha,Mbosoli amewataka wananchi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza katika zoezi hilo kwakuwa hatua hiyo ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu na kwamba asiyejiandikisha atakuwa amekosa haki na fursa ya kumchagua kiongozi anayemtaka.
Hatahivyo,awali kabla ya mafunzo hayo kufunguliwa washiriki walikula kiapo namba Sita na namba Saba vilivyohusu maafisa hao kutojihusisha na chama Cha Siasa ,Utii na uaminifu kilichoendeshwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha Joyce Mushi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.