Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakar Kunenge amewaasa wakazi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa tija ya uzalishaji Korosho na ufuta iakisi maisha ya wananchi mkoani humo yanabadilika na kuwa bora.
Akifungua mkutano wa wadau wa Korosho na ufuta kupitia tathmini ya maendeleo ya uzalishaji mazao hayo leo Februari 7, 2023 kwenye ukumbi wa "Flexi Garden Hotel" Wilayani Mkuranga, Kunenge aliwaasa wakazi wa mkoa huo kujipanga kutumia fursa ya ardhi yenye zaidi ya ekari laki 4.5 zilizopo wilayani Rufiji zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Katika kuendelea kuongeza uzalisha wa Korosho, Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wakurugenzi wa halmashauri mkoani humo kutenga na kutoa pesa za ununuzi wa vitalu huku akiwaelekeza wakuu wa wilaya kuorodhesha na kumpatia taarifa ya idadi ya ekari za ardhi na mahala zilipo zilizotengwa kwa ajili ya kwa ajili ya kuanzisha mashamba mapya ya Korosho akitolea mfano wa Halmashauri ya wilaya ya Rufiji ambayo tayari imetenga zaidi ya ekari 500.
Awali, mkuu wa wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir mbali na kueleza kuwa hakuna mkulima wa korosho wala ufuta anaedai malipo ya mazao waliyouza, pia alitaja baadhi ya changamoto kuwa ni mbadiliko ya tabia nchi ambayo alisema tafiti zinahitajika kukabiliana nayo ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wakulima huku akishauri mashirika ya Bima kuwa na uhakika wa kufidia wateja wao iwapo mazao yao yatakumbwa na changamoto.
Akizungumzia wakulima wa mazao ya korosho na ufuta, Nassir aliomba wasafirishaji wa vifungashio wawe wanashusha vya wilaya yake Mkuranga mjini badala ya kuvipeleka Rufiji.
Kwa upande wake Afisa Kilimo mkoa huo Jerry Mgonja akitoa taarifa alisema uzalishaji wa zao la ufuta mwaka 2021/2022 aliongezeka kufikia tani 11,629 na mauzo yalifanyika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Kuhusu uzalishaji wa zao la korosho Mgonja alieleza kuwa umeimarika kutoka tani 70,733 kwa mwaka 2020/2021 hadi tani 15,862 mwaka 2021/2022 huku ubora wa daraja la kwanza ukipanda kutoka asilimia 12 hadi 72.
Naye Meneja Mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha mkoa wa Pwani (CORECU) Hamisi Mantawela alisema wameendesha minada tisa ya korosho yenye tani 10,759,499 zilizouzwa kwa stakabadhi ghalani na tani 1,391,840 ziliuzwa kwa wabanguaji wa ndani.
Akitoa salaam za Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred aliwahimiza wakulima kusafisha mashamba yao wakati bodi hiyo ikiendelea na kujipanga tayari kwa ugawaji wa pembejeo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.