Waziri wa nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Mh Suleiman S. Jaffo amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuhahikikisha kuwa hakuna kituo cha Afya katika mkoa huo kinachopata nyota sifuri katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo ameyasema wakati wa uzinduzi wa wodi ya wazazi pamoja na jengo la huduma ya dharura katika hospitali ya wilaya ya Bagamoyo, Majengo hayo yamejengwa kwa ufadhili wa taasisi ya Dhinureyin Islamic Foundation iliyoko Mkoani Iringa.
Aidha amesisitiza juu ya utoaji wa huduma bora za Afya katika vituo vyote vya afya Mkoani Pwani na kuongeza kuwa hakuna sababu ya kituo chochote cha Afya nchini kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika Hatua nyingine Waziri Jaffo ameipongeza taasisi hiyo ya dini ya Dhi Nureyin kwa kuweza kujenga majengo hayo ya kisasa ambayo ni muhimu katika kutoa huduma ya Afya kwa jamii katika Mkoa wa Pwani.
Pia amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaj. Majid Hemed Mwanga kwa kuweza kufuatilia ufadhili na ujenzi huo kwa karibu zaidi hadi kufanikisha kupata majengo hayo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Mhandisi Evarist Ndikilo amesema kuwa kupatikana kwa majengo hayo ni ukombozi kwa wananchi wa wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kwani kumekuwa na ongezeko la msongamano wa wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura katika hospitali nyingi za Mkoa wa Pwani.
Mhandisi Ndikilo aliwataka wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa Afya nchini kuiga mfano wa taasisi ya DhiNureyin kwa kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za Afya.
Aidha Mwenyekiti wa Taasisi ya Dhi Nureyin Sheikh Said Abry amesema kuwa majengo hayo mawili yamegharimu kiasi cha shilingi millioni 703 za Tanzania na amesema mbali na ujenzi huo pia wamefadhili vifaa tiba vyote vitakavyowekwa ndani ya majengo hayo.
Sheikh Abry ameongeza kuwa taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia kuboresha sekta mbalimbali katika maeneo yote Nchini .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.