Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Evarist Ndikilo amesikitishwa na amechukizwa na matikeo ya kidato cha nne shule ya Sekondsari Hassanal Damji iliyoko kata ya magomeni ,katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kupata alama ya sifuri(zero) kwa wanafunzi 68 na utoro uliokithiri.
Kutokana na matokeo hayo ametoa miezi miwili kwa Mkuu wa Wilya ya Bagamoyo, Watendaji wa mitaa, Kata na Vitongoji kufuatilia chanzo kilichosababisha Wafunzi hao kufeli kiasi hicho wakati shule hiyo ina walimu 57 ambao wanatosha kutoa matokeo bora.
Akizungumza na viongozi , walimu na wanafunzi wa shule hiyo, wakati wa Ziara yake Mkoani hapi, Mhandisi Ndikilo alisema kuwa amesikitishwa sana na matokeo hayo hivyo kuna kila sababu ya kuchukua hatua mapema kurekebisha kasoro zilizopo ili shule iweze kutoa matokeo bora mwakani.
Aliwaasa wanafunzi hao kuacha utoro na kupotelea vichakani wakati wa vipindi badala yake wahudhurie masomo ili kuinua taalama zao na kuifanya shule yao kuwa na matokeo bora.
“Acheni kuchezea elimu kwani ni msingi na ufunguo wa maisha yao ya baadae,Mnakunywa uji shuleni, walimu wapo wa kutosha , kwanini wanafunzi hawahudhurii masomo”
“Matokeo haya si ya kufurahisha division two ni wanafunzi 2, division three ni wanafunzi 6 , na four wapo 72, na sifuri 68 ufaulu huu lazima tuuchukulie hatua ili wanafunzi waweze kufaulu zaidi” alisema Mhandisi Ndikilo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Ndikilo amewaagiza Wakuu wote wa Wilaya za Mkoa Pwani kufanya Msako wa Kuwasaka watoto wa jamii ya wafugaji ambao hawajapelekwa shule na kuhakikisha wanakwenda shule na si kubaki nyumbani na kujishughulisha na shughuli za uchungaji wa mifugo.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa alisema utoro shuleni hapo upo kwa asilimia 15 jambo ambalo sio zuri.
Alisema pia amejipanga kuanzisha kampeni ya TOKOMEZA UTORO ili kuondoa changamoto hiyo mashuleni hapo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.