Katibu Tawala mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania Rashid Mchata, amewataka watumishi wa umma kutambua mahitaji halisi na kero zinazowakabili wananchi na kuzitafutia majibu ili kukabiliana na wimbi la malalamiko ya upatikanaji wa huduma kwenye maeneo yao.
Mchata ametoa kauli hiyo Novemba 21, 2023 wakati akifunga mafunzo ya maafisa Tarafa na watendaji Kata kutoka Halmashauri zote za mkoa wa Pwani ambao wamepata mafunzo ya kujengewa uwezo wa namna ya kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, sheria na kanuni za utumishi wa umma.
Amesema mafunzo hayo siku mbili yaliyoandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo yanalenga kuwakumbusha watumishi hao namna bora ya kutimiza majukumu yao ili kuwahudumia wananchi ipasavyo.
“Badilisheni mitazamo hasi kuhusu kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yenu, kwa kufanya hivyo mtakuwa mmeisaidia sana serikali maana kwa sasa kuna utaratibu kila mkoa unatoa taarifa ya namna inavyoshughulia changamoto, na tumeona kero nyingi anazitatua Mkuu wa mkoa, ina maana kwenye maeneo yenu hamtimizi majukumu yenu inavyotakiwa, ninaomba mkawe majibu ya wananchi huku mkijitahidi pia katika suala la ukusanyaji mapato,” amesema Mchata.
Ameongeza kuwakumbusha watumishi hao kuwa miongoni mwa maeneo yenye migogoro mingi ni ya ardhi na kuwa baadhi ya viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji wamekuwa sio waaminifu, wanashirikiana na madalali kuuza viwanja ambavyo vinamilikiwa na watu au taasisi kisheria, wanawatapeli watu ni eneo la kushughulikia ili kumsaidia mkuu wa mkoa.
Zaidi ya maafisa tarafa na watendaji 150 wamepatiwa mafunzo hayo ambapo kwa awamu ya pili nchini yamefanyika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Dodoma, Mtwara, Lindi na Tabora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.