Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashidi Mchatta, ameanzisha rasmi mafunzo ya wataalamu watakaotekeleza Kampeni ya Msaada wa Kisheria Kwa Wote, inayosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria. Mafunzo haya yana lengo la kuwawezesha wataalamu kutoa elimu ya kisheria na kusaidia wananchi katika utatuzi wa migogoro mbalimbali.
Mafunzo hayo ya siku moja yanafanyika Kibaha, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, na baada ya kuyakamilisha, wataalamu hawa watawafikia wananchi katika halmashauri zote tisa za Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kutoa huduma ya msaada wa kisheria.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mchatta alisema kuwa mafunzo haya yanawajengea uwezo wataalamu hao ili kuhakikisha utekelezaji wa kampeni unafanyika kwa ufanisi na weledi.
Tutumie mafunzo haya kama fursa ya kutatua changamoto za msaada wa kisheria kwa wananchi. Kama kuna maeneo yanayohitaji ufafanuzi, tusisite kuuliza ili tuwe na uelewa wa pamoja utakaoleta tija katika kutatua masuala ya kisheria,†alisema Mchatta.
Aidha, alisisitiza kuwa huduma hii ni hatua kubwa ya serikali katika kusaidia wananchi, hasa wale wasio na uwezo wa kugharamia wanasheria au wanaoishi maeneo ya mbali, ili wapate msaada wa kisheria katika masuala ya ndoa, mirathi, ardhi, na ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Angela Anatory, alisema kuwa wananchi wengi wanahitaji msaada wa kisheria, lakini wanakumbwa na changamoto za umbali na ukosefu wa fedha, hivyo serikali imeona umuhimu wa kuanzisha kampeni hii.
Kampeni hii, inayojulikana kama Huduma ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), inatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 24 Februari 2025 katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Mailimoja, Kibaha. Tayari huduma hii imeshafanyika katika mikoa 19, na sasa Pwani inakuwa mkoa wa 20 kunufaika. Kampeni itaendelea kwa siku tisa, kuanzia 25 Februari hadi 5 Machi 2025, ikilenga kuwafikia wananchi wengi kadri inavyowezekana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.