Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchata, leo Mei 5, 2023 ametembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya maendeleo wilayani Mafia na kueleza kuwa kuna haja ya kuangaliwa upya gharama za ununuzi na usafirishaji vifaa katika wilaya hiyo.
Aliyasema hayo baada ya kubaini kuwa ununuzi wa vifaa na usafirishaji unagharama kubwa kulinganisha na maeneo mengine ya bara hali inayosababisha miradi mingi kuhitaji nyongeza ya pesa za ukamilishaji.
Akiwa Wilayani humo, Mchata ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania alitembelea na kukagua ujenzi wa miradi ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura (EMD) na mahututi (ICU) kwenye hospitali ya wilaya, ujenzi wa shule ya msingi Mrambani (vyumba 11, jengo la utawala, nyumba mbili za watumishi na vyoo matundu 24) na ujenzi wa barabara ya Kichangachui-Hutchery.
Akitoa taarifa ya Mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa dharura (EMD) na mahututi (ICU) kwenye hospitali ya wilaya ya Mafia, Mganga mkuu wa Wilaya hiyo Zuberi Nzige alieleza kuwa umetekelezwa kwa kutoka Serikali kuu za GoT-TCRP (UVIKO 19) na mchango wa halmashauri yote kwa pamoja ikiwa ni zaidi ya sh. Milioni 560.
Pamoja na majengo hayo, halmashauri hiyo imenunua vifaa vya kisasa vyenye viwango vinavyokubalika kimataifa vitakavyotumika kupima na kupata taarifa sahihi na za uhakika ya wagonjwa kisha kutoa tiba sahihi.
Alisema kuwa mradi huo unaolenga kusogeza utoaji huduma za afya na kupunguza vifo visivyo vya lazima kwa wagonjwa wa dharura na mahututi nakupunguza gharama za rufaa umekamilika kwa asilimia 100 na utakuwa na manufaa ya kutoa huduma kwa wagonjwa hao na kuhudumia si chini ya wananchi 66,180.
Mradi mwingine uliyokaguliwa na Mchata ni wa ujenzi wa shule ya msingi Mrambani ambako vimejengwa vyumba 11 vya madarasa, jengo la utawala, nyumba mbili za watumishi ambazo kila moja ina uwezo wa kukaliwa na kaya mbili za watumishi (two in one) na vyoo matundu 24 ambao hadi sasa umegharimu zaidi ya sh. Milioni 400 ambapo majengo mengine yamekamilika isipokuwa la utawala ambalo lipo kwenye hatua ya ghebo na nyumba hizo za waalimu ambazo ziko kwenye hatua ya umaliziaji.
Taarifa ya Mwalimu mkuu wa shule hiyo Saida Kilimo ilieleza kuwa chanzo cha fedha ya utekelezaji mradi huo ni za GPE LANES II, mchango wa wananchi pamoja na halmashauri.
Mwl. Kilimo alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo umesaidia kusogeza upatikanaji wa huduma ya elimu msingi kwa wanafunzi waliokuwa mbali na shule za msingi za Kilimahewa na Kigamboni, kuhakikisha kila mtoto anapata huduma ya elimu ya msingi na kuwa wakati wa utekelezaji mradi huo pia umetoa ajira za muda kwa wananchi.
Mchata pia alikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kichangachui-Hutchery yenye urefu wa kilomita 2.3 kwa kiwango cha lami ambao upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji ukiwa umegharimu karibu sh. milioni 900.
Mradi huo ambao upo katika hatua za mwisho unaotekelezwa chini ya TARURA na mkandarasi Gsix Investment Ltd. utarahisisha na kuunganisha huduma za kijamii za usafiri na usafirishaji wa uhakika kwa abiria na mazao ya wakulima, wavuvi na wafanyabiashara baina ya vitongoji mbalimbali vilivyopo ndani na nje ya mji wa Kilindoni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.