Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, imeagiza mikoa na wilaya kupitia kamati za maafa katika ngazi zote, kuainisha na kuandaa rasilimali za kuzuia, kuandaa na kukabiliana na maafa kama vile mvua za El nino.
Aidha serikali inaendelea kuchukua hatua za kuzuia madhara kufuatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA, mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli kwa kipindi cha mwezi oktoba hadi desemba 2023 kuonesha uwepo wa El- nino na kuendelea hadi Januari 2024.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Anderson Mutatebwa, Septemba 27,2023 kwenye ufunguzi wa kikao kazi cha kuimarisha uwezo wa kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El nino kwa kamati ya usimamizi wa maafa mkoa wa Pwani.
Amesema kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa maafa, namba 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake ambayo imeanzisha kamati za usimamizi wa maafa kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, kata na vijiji kuzuia na kupunguza madhara ya majanga ya aina zote na kujiandaa kurejesha hali kwa ubora zaidi endapo maafa yatatokea.
“Tumekutana leo kukumbushana wajibu muhimu kwa kila mmoja kuwajibika katika eneo lake ili kuokoa maisha na kulinda mali zawananchi , tukumbuke mkoa unaingia kusaidia juhudi za halmashauri husika kwa kushirikiana na wananchi kwenye maeneo yao kwa ajili ya kuokoa maisha na mali za jamii zetu kutokana na maafa,” Mutatebwa.
Amesema mikoa 14 nchini kufikiwa kwa ajili ya kupata elimu ya namna ya kukabiliana na mvua za El nino kama vile Pwani( ikiwemo visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Kagera, Tanga, Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Morogoro na Kigoma hadi kufikia Septemba 30.
Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani, Rashid Mchata amesema tayari mkoa huo una kamati za maafa kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji na kwamba wamejiandaa vyema kukabiliana na majanga ikiwemo mvua za El nino.
Amesema suala la kukabiliana na majanga kwao ni endelevu na kwamba watahakikisha kamati za maafa zina uwezo wa kifedha ili kutekeleza majukumu yao kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kuwa salama.
“ Uwezekano wa kutokea kwa mvua za El nino mkoani kwetu upo kwa sababu ya historia katika miaka ya nyuma lakini pia tumezungukwa na mito na bahari, tumejiandaa na tumefanya maandalizi ili kukabiliana na majanga hayo amesema Mchatta.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.