Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amewataka watendaji wanaotekeleza program mbalimbali za Elimu ya watu wazima na wale wanaopata elimu nje ya mfumo kuweka vipaumbele vitakavyoendana na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025.
Prof. Mkenda ameyasema hayo octoba 13, 2023 kwenye kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu ya watu wazima ambalo kitaifa limefanyika mkoani Pwani.
Amesema serikali ilianza programu ya watu wazima kwa lengo la kuwasaidia wananchi kupata ujuzi utakaowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha na kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
“Kila mmoja ni shahidi wa mafanikio yanayotokana na program hii ya elimu ya watu wazima ambayo ilianzishwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere akilenga kuwasaidia waliokosa nafasi ya kupata elimu kurudi shule kujiendeleza na wamefanikiwa kujua kusoma, kuandika na kuhesabu pamoja na uwezo wa kufanya shughuli za ujasiriamali,” amesema Prof. Mkenda.
Amewakumbusha watendaji wanaosimamia program ya elimu ya watu wazima kuhakikisha inapatikana kwenye maeneo yote nchini na vituo vinavyoisimamia vitambulike.
Awali, Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, anayeshughulikia Elimu, Dk. Charles Msonde amesema serikali imewapa jukumu la kutekeleza sera ya elimu kuanzia ngazi ya elimu Msingi hadi watu wazima.
Amesema katika kutekeleza sera ya elimu, wamebaini changamoto mbalimbali kama vile baadhi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la kwanza hadi la nne kutokujua kusoma, kuandika wala kuhesabu.
Ameongeza kuwa kuna changamoto ya umaahiri wa lugha ya kiingereza kwa wanafunzi wa sekondari ambapo matokeo ya mwaka 2022 ya wanafunzi milioni 1.7 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza ni asilimia 29 ndio waliofaulu somo hilo huku umahiri wa lugha hiyo ukiwa mdogo kwa asilimia 71 ya wanafunzi wengine.
Amesema baada ya kubaini tatizo hilo, walianzisha utekelezaji wa malengo ya muda mfupi na mrefu kwa kuanzisha program za kuwajengea uwezo wanafunzi hao kujiamini na kuweza kuongea lugha ya kiingereza.
“Baada ya kuanza kutekeleza mpango huo kuanzia mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, asilimia 96 ya wanafunzi wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu, darasa la pili ni asilimia 99 na wanafunzi wa kidato cha kwanza ndani ya miezi minne hadi mitano wamefundishwa umahiri wa kujua kuandika na kuzungumza kiingereza,” amesema Msonde.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema wanafunzi 1943 wanaendelea na elimu ya watu wazima huku wanakisomo 2080 wakisoma masomo ya uzalishaji mali kama vile ususi, kilimo, utengenezaji wa batiki na shughuli nyingine za mikono ambazo zinawaingizia kipato.
Amesema mpango huo pia umewasaidia vijana kujiunga na vyuo vya ufundi stadi kwa ajili ya kupata ujuzi wa aina mbalimbali na kwamba katika program ya elimu ya masafa kwa mkoa huo, jumla ya wanafunzi 1013 wanaendelea na masomo.
“Licha ya jitihada zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha elimu ya watu wazima inakuwa na tija kwa jamii, zipo baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa program ikiwamo walimu wa kujitolea kutopata mafunzo ya MEMKWA, wawezeshaji kutolipwa stahiki zao, uhaba wa vitendea kazi kama vile vitabu na miongozo,” ameeleza Kunenge.
Aidha amebainisha mikakati ya mkoa kuwa ni kupunguza idadi ya wasiojua kusoma kuandika na kuhesabu, kuihamasisha jamii kutowatenga watoto wa kike walionufaika na program hiyo wanapohitimu masomo na kurudi nyumbani badala yake wawape ushirikiano ikiwemo kuwatafutia ajira.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.