Serikali Mkoani Pwani imeeleza kuwa itayafutia umiliki mashamba makubwa ambayo hayajaendelezwa na kuyagawa kwa wakulima wanaolima zao la mkonge ili kufufua zao hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa ziara ya Mhe. Kasimu Majaliwa (Mb)Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Tanga.
"Tunakwenda kutekeleza maelekezo yako Mhe. Waziri Mkuu ya kufufua zao la Mkonge, nitume salaamu kwa wamiliki wa mashamba makubwa Mkoa wa Pwani yasiyoendelezwa, maelekezo ya Serikali ni kuyafutia umiliki na kugawa kwa wakulima walime Mkonge" alisema Mhandisi Ndikilo.
Awali akitoa hali ya Uzalishaji wa zao hilo katika Mkoa wa Pwani Ndikilo, amemshukuru Mhe. Waziri Mkuu kwa kuutambua Mkoa wa Pwani kama wadau muhimu wa zao hilo na kuwaalika katika ziara hiyo.
Ndikilo alieleza kuwa kwa sasa Mkoa wa Pwani una mashamba makubwa mawili ya Mkonge yanayo milikiwa na Ubena Highland Estate lililopo Chalinze na shamba la Mohamed Enterprises lililopo Kibaha ambapo jumla ya Hekta 10,007 zimelimwa kwenye mashamba yote mawili na kwa msimu wa 2019/2020 wamefanikiwa kuzalisha tani 2,136 za mkonge.
Hata hivyo Ndikilo ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika zao hilo Mkoani Pwani ambapo ameeleza kuwa kupitia mashamba ya Mkonge yaliyopo Mkoa hapa umetengenza ajira 1,200 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
"Tunayo maeneo yanayofaa kwa Kilimo cha Mkonge na maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa kiwanda cha magunia fursa hizi tumezianisha kwenye mwongozo wetu wa Uwekezaji (Pwani Investment Guide) tunawakaribisha wawekezaji kuwekeza Pwani."
Mhe. Waziri Mkuu amefanya ziara ya siku moja MkoaniTanga pamoja na mambo mengine amefungua Jengo la Makao Makuu ya Bodi ya Mkonge Tanzania na kukutana na wadau wa Mkonge, baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Viongozi wengine Serikali, Wawekezaji na Vyama vya Wakulima wa Mkonge kwa lengo la kuhamasisha Kilimo hicho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.