Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na Programu ya Shule Bora na EdTech umeendesha warsha ya siku moja kwa ajili ya kuwajengea uwezo wataalamu kutoka Sekretarieti ya Mkoa pamoja na Halmashauri za Kibiti na Rufiji, kuhusu mfumo unaopendekezwa wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa Holiday Inn jijini Dar es Salaam, ikiratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa lengo la kuongeza uelewa wa wataalamu juu ya matumizi ya taarifa sahihi na mbinu bora za kuelimisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nazo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mwalimu Albert Machua aliishukuru Programu ya Shule Bora na EdTech kwa kufanikisha warsha hiyo muhimu, na kupongeza washiriki kwa ushiriki wao wa kina na michango waliyoitoa katika kujenga mifumo madhubuti ya tahadhari kwa jamii.
“Mafunzo tuliyoyapata yatatusaidia sana katika maeneo yetu kujiandaa na kukabiliana na majanga mbalimbali. Ni muhimu tuendelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutafsiri taarifa hizi, ili waweze kuchukua tahadhari mapema,” alisema Machua.
Aidha, alieleza kuwa matukio ya majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa yameendelea kujirudia mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani, hivyo ni muhimu kuchukua hatua za mapema, kwa kuwa hakuna njia ya kuyaepuka bali ni kuyakabili kwa maandalizi ya kitaalamu na ya kijamii.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Kiongozi wa Programu ya Shule Bora, Ndugu Flavian Lihwa alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Mkoa wa Pwani katika kukabiliana na majanga yanayoathiri miundombinu ya shule na utoaji wa elimu. Alisisitiza kuwa Programu ya Shule Bora itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali katika kuimarisha mifumo ya kupunguza athari za majanga kwenye sekta ya elimu.
Warsha hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za Mkoa wa Pwani kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya elimu na maendeleo ya jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kutumia mifumo jumuishi ya taarifa, elimu na teknolojia
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.