Timu ya Kiluvya United ya Mkoa wa Pwani imefanikiwa kupata klabu rafiki ya TAMPERE ya nchini Finland, itakayofanya nayo mashirikiano katika kukuza vipaji, mbinu za uchezaji na benchi la ufundi ili kuinua soka Mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo ndiye amefanikisha kuanza kwa ushirikiano huo, kati ya klabu ya Tempere iliyopo ligi kuu nchini Finland na Kiluvya United.
Aidha Mkuu wa Mkoa ametoa kiasi cha shilingi milioni moja kwa timu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza ili kuhakikisha inaingia ligi kuu.
Mhandisi Ndikilo alitoa mchango huo alipoitembelea timu hiyo kwenye kambi yake iliyopo kwenye shule ya Filbert Bayi iliyopo Wilayani Kibaha.
Alisema kuwa ili kufanikisha timu hiyo kupanda ligi kuu, wadau wa soka wa Mkoani Pwani wanapaswa kuichangia kwa hali na mali ili ifikie lengo hilo.
“Kiluvya United ni timu yetu ya Mkoa na endapo itapanda ligi kuu itauletea sifa Mkoa wetu na pia vijana wetu wataweza kuonekana na kufikia hatua ya kuichezea timu ya Taifa,” alisema Mhe Ndikilo.
Aidha alisema kuwa ili kuunga mkono masuala ya michezo ambayo ni ajira wadau hawana budi kuwaunga mkono ili kuwapa hamasa waweze kufanya vizuri.
Mhe. Ndikilo aliwataka wachezaji hao wacheze kufa na kupona ili kupanda kwenye ligi kuu.
Nae Katibu wa timu hiyo Bw. Sadiki Chonjo alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwaunga mkono na kuwapatia fedha hizo kwani zitasaidia kupunguza makali ya changamoto ya fedha.
Alisema timu yao inakabiliwa na changamoto kubwa ya fedha ambapo inahitaji zaidi ya milioni 10 kwa ajili ya kuiandaa timu yao.
Chonjo alisema kuwa wakifanikiwa kupata fedha hizo zitawasaidia kufanikisha harakati zao za kwenda ligi kuu.
Alieleza kuwa, timu hiyo ya Kiluvya United ipo daraja la kwanza ngazi ya Taifa na kwamba sasa katika kundi lake lenye timu nane, inashika nafasi ya tatu ikitanguliwa na Ruvu JKT na African Lion.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.