Katika jitihada za kuinua ufaulu wa masomo ya Kiingereza na Hisabati, Programu ya Shule Bora imeandaa mafunzo maalum ya siku mbili kwa walimu, yakiangazia mbinu bora za ufundishaji na kubadilishana uzoefu.
Mafunzo hayo ni ya siku mbili na yalianza tarehe 6 Machi 2025, katika Ukumbi wa Stella Maris, Bagamoyo, yakihusisha washiriki 156, wakiwemo walimu wa Kiingereza (36), walimu wa Hisabati (36), walimu wakuu (36), maafisa elimu kata (9), wathibiti ubora wa shule (18), waratibu wa Shule Bora kutoka halmashauri (9), pamoja na maafisa elimu taaluma wa mkoa wa Pwani.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijadili na kushirikiana katika, kuboresha mbinu za ufundishaji ili kuwasaidia wanafunzi kuelewa masomo kwa urahisi zaidi, kubadilishana uzoefu wa ufundishaji na ujifunzaji wa Kiingereza na Hisabati, kuandaa mpango kazi wa kuinua ufaulu wa masomo hayo katika mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoa wa Pwani, N’gwigulu Kube, amesema mafunzo haya yanalenga kuwawezesha walimu kubadilishana uzoefu na kuboresha mbinu zao za ufundishaji ili kuinua ufaulu wa wanafunzi.
“Mafunzo haya ni fursa kwa walimu si tu kujifunza mbinu mpya, bali pia kushirikiana na wenzao kubadilishana uzoefu wa ufundishaji. Ingawa wengi wamekuwa kwenye taaluma kwa muda mrefu, kujengeana uwezo mara kwa mara ni muhimu ili kuboresha matokeo ya wanafunzi” alisema Ng’wigulu.
Akifungua mafunzo hayo Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Jimmy Nkwamu, ameishukuru Programu ya Shule Bora kwa mchango wake wa kuandaa mafunzo hay ohayo ambayo yamekuwa yakiimairisha elimu mkoani Pwani.
“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yatawasaidia walimu kuongeza bidii na juhudi katika kazi zao, na nawasihi muwe mfano bora kwa wenzao na kuhakikisha mnatekeleza yale mliyojifunza” alisema Nkwamu.
Aidha, aliwakumbusha walimu wote mkoani Pwani kuzingatia taratibu na kanuni za Utumishi wa Umma katika utendaji wao wa kila siku.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.